
WANAJESHI wawili wa Jeshi la Ulinzi la Tanzania (JWTZ), wameuawa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kwa mujibu wa jeshi la Tanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ na kusainiwa na Kanali Gaudentiud Ilonda, leo tarehe 2 Februari 2025, imeeleza kuwa askari hao wawili, walikuwa wakilinda amani katika eneo la mashariki mwa DRC.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, askari wengine wanne wamejeruhiwa katika shambulio lililofanywa na waasi wa M23, katika mji wa Sake na Goma.
Taarifa ya Kanali Ilonda ilisema, “kufuatia mashambulizi ya mfululizo katika maeneo ya Sake na Goma yaliofanywa na waasi wa M23 tarehe 24 na 28 Januari, jeshi la ulinzi la Tanzania, limewapoteza askari wake wawili na wengine wanne kujeruhiwa.”
Alisema, “majeruhi wanaendelea kupata matibabu mjini Goma. Taratibu za kusafirisha miili ya marehemu pamoja na majeruhi zinaendelea kupitia sekretariati ya SADC.”
Aidha, jeshi limesema, vikundi vya wanajeshi wa Tanzania vilivyopo nchini DRC, vipo salama, imara na vinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa maelekezo ya uongozi wa SADC.
Mataifa yaliopoteza wanajeshi nchini Congo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa baada ya mkutano wa dharura wa Jumuiya ya mataifa ya Afrika Kusini mwa Afrika (SADC), siku ya Ijumaa, 31 Januari, mjini Harare nchini Zimbambwe.
Rais wa Zimbabwe na mwenyekiti wa SADC, Emmerson Mnangangwa alisema, hadi kufikia jana (tarehe 31 Januari), wanajeshi kutoka Malawi, Afrika Kusini na Tanzania walifariki katika makabiliano na kundi la M23, linaloungwa mkono na Rwanda.
Hadi sasa, Afrika Kusini imetangaza kuwapoteza wanajeshi 14 baada ya mmoja kuthibitishwa kufariki hospitalini usiku wa Jumamosi.
Hata hivyo, viongozi wa jumuiya hiyo wamekiri kuwa kikosi cha SAMIDRC kilichoanza kazi baada ya kuondoka kwa kikosi cha jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) cha EACRF, hakijatimiza majukumu yake ya kazi.
Lakini wamesisitiza, kitengo cha usalama cha TROIKA kinachooongozwa na Tanzania katika SADC kinatarajiwa kufanya kikao cha dharura kutafuta mbinu za kuwaleta pamoja wahusika wote kwenye mzozo wa mashariki mwa DRC kuhakikisha kwamba vita vinasitishwa.
Jeshi la Tanzania limekuwa likishiriki shughuli za ulinzi wa amani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa (UN) na jumuiya za kikanda ikiwemo, nchini Lebanon, Sudan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Liberia, Msumbiji Congo-DRC.
ZINAZOFANANA
Rais Mwinyi amuapisha Kamshna mpya wa ZRA
Mtanzania achaguliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini
Usalama mtandaoni ni amani kwa Taifa