WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima amewaasa wananchi kuacha kudanganyika na imani za kishirikina kwa imani za kupata mafanikio. Anaripoti Mwandishi Wetu, Nzega, Tabora … (endelea).
Waziri Dk. Gwajima ameyasema hayo leo tarehe 23 Oktoba, 2024 wakati akizungumza na wananchi, kwenye Wilaya za Igunga na Nzega mkoani Tabora katika ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema matokeo ya imani hizo yanasababisha vitendo vya ukatili wa kijinsia na kwa watoto kuongezeka nchini, hasa ubakaji, ulawiti na mauaji hali inayoleta taharuki kwenye jamii kutokana na athari za maumivu na vifo.
“Waganga wa kienyeji wasiotambulika wanawadanganya kufanya mambo ya ajabu na ndio sababu wanafanya tiba zao kwa kificho. Pambaneni kufanya kazi badala ya kudanganywa na waganga hao,” amesema Dk. Gwajima.
Ameongeza kuwa, Serikali inapambana na ukatili ambao matokeo yake ni pamoja na kukosa huduma za msingi kama shule, zahanati, barabara, fursa za mikopo na maji, sekta ambazo zinatafsiri maendeleo na ustawi wa jamii na ndio zinazinduliwa katika ziara hiyo.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha amebainisha baadhi ya matukio yaliyotokea hivi karibuni ikiwemo la binti kufariki wilayani humo baada ya kutolewa mimba ambapo wahusika wote wamekamatwa.
Mhe. Chacha amesema mkoa kupitia vyombo vya usalama, unashughulika kikamilifu na watuhumiwa wa ukatili na watahakikisha wanafikishwa kwenye mikono ya sheria wote watakaobainika.
Katika ziara hiyo katika Wilaya za Igunga na Nzega, Waziri Dk. Gwajima amekagua na kuzindua madarasa Shule ya Sekondari Mwayunge na Zahanati ya kijiji cha Nguriti wilayani Igunga na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa kalavati kwenye Kata ya Ijanija, Wilaya ya Nzega na miradi yote imegharimu jumla ya Sh. 500.5 milioni.
ZINAZOFANANA
Benki ya NBC yatambulisha kampeni ya Kilimo Mahususi kwa wakulima na wafugaji Mbeya
Upelelezi wakwamisha kesi ya Boni Yai
Wahitimu 417 kutunikiwa vyetu ITA