MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekabidhiwa rasmi ya rada zake mbili za hali ya hewa zilizopo Mwanza na Dar es salaam zilizokuwa zinafanyiwa uboreshaji na kampuni ya Enterprises Electronic Corporation (EEC) kutoka Alabama, Marekani (USA). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Maboresho hayo yaliyofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia bajeti ya maendeleo yalilenga kuboresha (upgrading) ufanisi wa rada hizo zilizokwisha tumika kwa zaidi ya miaka 10 kwa kutoa vifaa vyenye teknolojia yenye software ya kizamani (edge 5) na kufunga ya kisasa (edge 6) ili kupata picha nzuri itakayoweza kutafsiriwa kiurahisi.
Maboresho hayo ni muhimu kwani yatawezesha kuendana na teknolojia inayotumika katika rada nyingine za hali ya hewa zilizofungwa hivi karibuni katika mikoa ya Mtwara, Mbeya na Kigoma na hivyo kutumika katika mfumo jumuishi wa rada (MOZAIC).
Katika makabidhiano hayo yaliyofanyika katika ofisi za rada ya Dar es Salaam, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu TMA ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa TMA, OFISI YA Zanzibar, Masoud Faki alisema amefuatilia kwa karibu muonekano wa picha za rada ya Bangulo, Dar es Salaam, ameonesha kuridhishwa kwa maboresho ya vifaa vilivyohuishwa na kufanya rada hizo kuwa na uwezo mzuri wa kuona matukio ya hali mbaya ya hewa kwa maeneo ya Pwani ya Kaskazini ikiwemo vimbunga endapo vitajitokeza Baharini ili kuwatahadharisha wakazi wa eneo husika.
“Kwa kweli nimeridhishwa na namna ambavyo hizi ‘instruments’ (vifaa) zimekuwa ‘replaced’ na kuona sasa rada zinaweza kufanya kazi kwa kupata ‘product’ (picha) zenye ‘high resolution’ (muonekano mzuri) hadi baharini hivyo tunatarajia zitatusaidia katika ku ‘predict’ (kutabiri) hali mbaya ya hewa ili kuokoa jamii yetu dhidi ya majanga ya hali mbaya ya hewa,” alisisitiza Masoud.
Masoud aliongezea kwa kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea na uboreshaji wa miundombinu ya hali ya hewa ikiwemo ununuaji na ufungwaji wa rada tatu za hali ya hewa katika mikoa ya Mtwara, Kigoma na Mbeya na kufanya kuwa na jumla ya rada tano mpaka sasa ikiwa ni matazamio ya kufikia mtandao wa rada saba hapa nchini.
Kwa upande wa mwakilishi wa kampuni ya EEC nchini Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi kutoka kampuni ya INFRATECH LIMITED (IFL), Edwin Kasanga wakati akikabidhi mradi huo alisema jukumu lao la kuziboresha rada hizo za hali ya hewa kwa kuzifanya ziwe za kisasa na zenye ufanisi mzuri, kwa upande wa Mwanza walikamilisha mwezi Julai wakati Dar es Salaam wamekamilisha mwezi Oktoba 2024.
Aidha, Kasanga aliwaomba Wahandisi wa TMA kuitumia elimu waliyoipokea nchini USA kupitia mafunzo ya kujengewa uwezo na watengenezaji kwa kuhakikisha wanazitumia rada hizo ipasavyo pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya programu hizo za kisasa.
Rada hizi zinauwezo wa kufuatilia matukio ya hali ya hewa kwa umbali wa nusu kipenyo cha zaidi ya kilomita 250.
ZINAZOFANANA
Ujenzi wa barabara, madaraja Babati kufungua Utalii
Mradi wa Nishati Safi wa EWURA kupunguza madhara ya kuni kwa jamii
TCC yaibuka kidedea tuzo za PMAYA Dar