WAKENYA wamefungua ukurasa mpya baada ya bima mpya ya afya kuanza kutumika leo, ambayo inatoa fursa ya matibabu kwa wananchi wote. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Akizindua rasmi mpango na bima hiyo mpya ya afya katika Kaunti ya Kakamega, Waziri wa Afya wa Kenya, Debra Barasa, amesema lengo la serikali ni kuwapa huduma za afya Wakenya wote.
Mapema wiki hii, Kamati ya Afya ya Bunge, iliupa ridhaa mpango huo mpya baada ya hoja za kamati hiyo kuhusu utendakazi kujibiwa.
Awali, kulikuwa kumetajwa mapungufu kwenye mfumo mzima wa jinsi ya kubaini kiwango cha fedha watakazochangia wasiokuwa na ajira rasmi, huku wale wenye ajira rasmi wakikatwa asilimia 2.75 ya mshahara, ili kuchangia kwenye bima hiyo mpya inayoitwa kwa kifupi SHIF.
Inaelezwa kuwa kiwango hicho ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na mpango wa awali wa Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF), ambao waliokuwa na mishahara mikubwa walilazimika kuchangia Sh. 1,700 za Kenya, kinyume na mfumo mpya wa SHIF.
Mfumo wa SHIF umezinduliwa baada ya kufanyiwa majaribio katika Kaunti za Turkana, Tana River, Narok, Migori, Bungoma, Bomet, Kiambu na Nairobi, ili kubaini vigezo vya kuchangia vya wasiokuwa na ajira rasmi.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), Elijah Wachira, amewaondoa hofu wananchi na kusema hakuna Mkenya atakayekosa huduma wakati ambapo mfumo wa bima unachukua sura mpya.
Mfumo huo mpya unawapa wanachama wa NHIF na wananchi wengine, nafasi ya kusajiliwa na Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), ili waweze kupata huduma wanazohitaji.
Kuanzia leo tarehe 01 Oktoba 2024, kila mteja wa hospitali za umma aliyekuwa anatumia bima ya NHIF, analazimika kusajiliwa upya na SHA na kwamba lengo ni serikali ni kukusanya Sh. 148 bilioni kwa mwaka kupitia mfumo huo mpya wa bima ya SHIF.
Hata hivyo, Seneta Okiya Omutata, wa Kaunti ya Busia, amewasilisha malalamiko rasmi mahakamani kupinga utekelezaji wa bima ya SHIF kwa madai kuwa inakosa sheria mahsusi ya kuitekeleza.
ZINAZOFANANA
Putin, Pezeshkian waahidi kuimarisha uhusiano
Gachagua kunyoa au kusuka Bunge la Seneti wiki ijayo
Watu 78 wafariki baada ya boti kuzama Kongo, 58 waokolewa