December 27, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mbowe amdai Msigwa Sh. 5 bilioni

 

FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ametoa siku tano kwa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Kanda ya Nyassa, Mchungaji Peter Msigwa, kuomba radhi na kulipa fidia ya Sh. 5 bilioni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mbowe anadai kiasi hicho cha fedha kwa madai ya kukashifiwa na kuvunjiwa hadhi,kutokana na matamshi ya Msigwa yaliyotolewa hadharani baada ya kuondoka Chadema na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kwa mujibu wa barua yake ya tarehe 2 Septemba 2024, iliyosainiwa na mawakili wa kampuni hiyo, wakiongozwa na Hekima Mwasipu, kutokea kampuni ya Matwiga Law Chambers, Mbowe anadai matamshi ya Msingwa yamemchafua mbele ya jamii.

Mwasipu anasema, Msigwa alidai kuwa Mbowe ameanzisha “Mbowe Foundation na anatumia chama cha Chadema kwa manufaa yake binafsi. Alieleza haya kupitia mikutano ya hadhara, vyombo vya habari na hata mitandao ya kijamii.”

Katika moja ya mikutano yake, Msigwa alisema, “Mbowe amegeuza Chadema kuwa SACCOS yake; fedha za chama zinaishia kwenye taasisi binafsi.”

Mawakili wa Mbowe wameeleza kuwa matamshi hayo yameathiri sifa ya Mbowe ndani na nje ya Tanzania, hasa kutokana na nafasi zake mbalimbali kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuwa Naibu Mwenyekiti wa Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia vya Afrika (DUA).

Hata hivyo, Msigwa amejibu madai ya Mbowe na mawakili wake kwa kusema, hayuko tayari kuomba radhi wala kulipa chochote ambacho mwanasiasa huyo wa upinzani amekidai.

“Sina cha kuomba radhi. Sina. Nitaendelea kusimamia maneno yangu na kauli zangu hadi mwisho. Kama Mbowe anaona amekashifiwa, basi apelike malalamiko yake mahakamani. Nitakwenda huko kuthibitisha kile nilichokieleza,” ameeleza Msigwa katika mahojiano yake na MwanaHALISI Online.

Amedai kuwa anaweza kuthibitisha kile anachokise. Alikuwa akijibu swali la mwandishi aliyetaka kufahamu, msimamo wake kuhusiana na jambo hili.

About The Author

error: Content is protected !!