MATUKIO ya madai ya wanaume kupokwa sehemu zao za siri – nyeti – yakiwa yanashamiri hapa Zanzibar, tayari yamesababisha umwagikaji damu baada ya kijana wa umri wa miaka 35 kushambuliwa hadi kufa kwa tuhuma za kumshika bega mtu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea). Hamad Othman Mwalim, mkaazi wa Jojo Majimbikani, Wete, Kaskazini Pemba, amethibitishwa kuwa aliuawa baada ya kushambuliwa na watu waliodai mwenzao alishikwa bega na Hamad na kumsababishia “nyeti” yake kutoweka. Ni tukio lililotokea tarehe 10 Aprili eneo la Madenjani, Wilaya ya Wete, ambako Hamad alikuwa safarini akirudi nyumbani kwao akitokea Ole. Familia yake inasema anaishi Unguja na kwamba alifika Pemba kusalimia ndugu na jamaa zake. Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, imethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa inawashikilia watu saba na kuahidi kuwa watapelekwa mahkamani mara baada ya uchunguzi kukamilika. Taarifa hiyo inakuja wakati Kamishna wa Polisi Zanzibar {CPZ}, Kombo Khamis Kombo, akiviambia vyombo vya habari kuwa watu wapatao 40 wamekamatwa na upelelezi dhidi yao unaendelea kutokana na jumla ya matukio 29 yaliyokwishatokea maeneo mbalimbali Unguja na Pemba. Kamishna Kombo amesema kwamba matukio hayo yanahusu tuhuma za kujitokeza wanaume wakidai “nyeti” zao zimetoweka baada ya kushikwa bega na wanaume wenzao. Kamishna Kombo amesema madai hayo yanahusishwa na imani za kishirikina kwa sababu wale wachache waliochunguzwa, akiwemo mtuhumiwa aliyetaka kusababisha uvunjaji wa amani eneo la Madungu, Chake Chake, Pemba, baada ya kudai nyeti zao zimepotezwa, wamekutwa wanazo. Kamishna Kombo aliyekutana na waandishi wa habari ofisini kwake Ziwani, yalipo makao makuu ya Polisi Zanzibar, amesema mikoa yote mitano, mitatu Unguja na miwili Pemba, tayari kumeripotiwa kutokea matukio hayo. Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, unaongoza kwa matukio hayo, likiwemo lile la kijana wa sekondari aliyekimbilia kwa mama yake mzazi eneo la Kinuni, baada ya kubaini “nyeti” zake zimepotea baada ya kuguswa bega na mtu ambaye hakumfahamu. Mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania {TRA} aliyepo Zanzibar, Hassan Yunus, alijeruhiwa vibaya hivi karibuni baada ya kushambuliwa na watu waliojitokeza mbele yake alipokuwa ameingia Setendi Kuu ya Mabasi Kijangwani, wakidai alimshika bega kijana mwenzao kwa nia ya kuchukua nyeti yake. Hassan akisimulia mkasa uliomkuta kupitia video iliyoenea mitandaoni, alidai waliomshambulia ni katika vijana aliowakuta pembeni eneo la Kariakoo, alipokuwa duka la wakala wa pesa akimtumia pesa ndugu yake. “Naona wale vijana waliokuwa karibu na dukani nilipokuwa natuma pesa, walifuatilia baada ya kuondoka pale. Nilishtukia waliponikaribia ndani ya stendi ya mabasi huku mmoja akisema ndiye huyu aliyekushika bega. “Ghafla nikaanza kushambuliwa lakini baadhi ya wale vijana haraka walishikilia mkoba wangu na kutoweka nao. Mulikuwa na Shilingi milioni tano wameziiba na kutoweka,” alisema. Ilikuwa bahati yake mashambulizi yalisita mara alipotokea mtu mmoja aliyemtambua na kuasa huyo ni mfanyakazi wa TRA anayemjua na kama kuna tatizo lolote la kutuhumiwa, basi apelekwe Kituo cha Polisi badala ya watu kujichukulia sheria mkononi. Hamad alipelekwa Kituo cha Ng’ambo akiwa anavuja damu mwili mzima na ikionesha kuumia zaidi kichwani. Wakati huohuo, mtuhumiwa Salum Omar mkaazi wa Matale kisiwani Pemba, amehuhumiwa kifungo cha miezi mitatu au faini ya Sh. Laki moja baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kusababisha uvunjifu wa amani. Kwa mujibu wa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Zanzibar, ZBC, Hassan Mselem, hukumu hiyo ilitolewa juzi na Mahkama ya Mwanzo ya Chake Chake, Pemba, kufuatia mtuhumiwa kukiri kosa mahkamani la kutoa kauli ya kuwa alishikwa bega. Awali alidaiwa na karani wa mahkama kuwa alihatarisha maisha ya mwananchi kwa kutoa kauli kuwa aliguswa bega na nyeti zake kutoweka. Mtuhumiwa alipopelekwa Polisi Madungu, alikutwa hana hitilafu yoyote ya viungo vyake. Share this… Facebook Pinterest Twitter Linkedin Whatsapp About The Author Erasto Masalu See author's posts Post navigation Askofu Mfumbusa wa jimbo la Kondoa afariki dunia