Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Juma Zuberi Homera

 

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Juma Zuberi Homera, amewataka wajumbe wa bodi za wadhamini nchini kuzingatia kikamilifu sheria, uwajibikaji na uadilifu katika usimamizi wa mali za taasisi wanazoziongoza, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni msingi muhimu wa kuimarisha utawala bora na kuchochea maendeleo endelevu ya jamii. Anaripoti Mwandishi Wetu, Songea … (endelea). 

Akifungua mkutano wa wajumbe wa bodi za wadhamini ulioandaliwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na kuwakutanisha washiriki kutoka mikoa ya Ruvuma, Njombe, Mtwara na Lindi katika Ukumbi wa Familia Takatifu, Bombambili Manispaa ya Songea jana,Waziri Homera alisema bodi hizo zina jukumu kubwa la kusimamia na kulinda rasilimali za taasisi kwa manufaa ya wanachama na jamii kwa ujumla wake.

Alisisitiza kuwa nafasi ya udhamini siyo heshima pekee, bali ni dhamana nzito inayohitaji uwajibikaji wa hali ya juu. “Ni wajibu wa kila mdhamini kuhakikisha mali za taasisi zinalindwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa, si kwa maslahi binafsi,” alisema.

Aidha, Waziri Homera alibainisha kuwa licha ya uwepo wa sheria, kanuni na miongozo, bado baadhi ya bodi za wadhamini zinakabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo ubadhirifu wa mali, migogoro ya kiuongozi na kushindwa kuzingatia katiba zao. Alionya kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote watakaokiuka misingi ya utawala bora.

Katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi, Waziri huyo aliiagiza RITA kuongeza kasi ya maboresho ya mfumo wa kidijitali wa eRITA ili uwe rafiki zaidi kwa watumiaji, pamoja na kuanzisha huduma za mkoba (mobile clinics) zitakazowafikia wadau walioko maeneo ya pembezoni.

Katika hatua nyingine, Waziri Homera alipongeza mafanikio ya RITA katika utoaji wa vyeti vya kuzaliwa na vifo ndani ya saa 48 kupitia mfumo wa eRITA, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 94 ya maombi yanakamilishwa ndani ya muda huo. Mafanikio hayo yameelezwa kuwa ni hatua kubwa katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi wa taasisi.

Kwa upande wake, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi, alisema mkutano huo, wenye kaulimbiu ya “Uwajibikaji wa Bodi za Wadhamini kwa Ulinzi wa Mali za Taasisi na Maendeleo ya Jamii,” ni sehemu ya mkakati wa wakala huo wa kuwajengea uwezo wajumbe wa bodi za wadhamini ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo.

Alisisitiza kuwa bodi za wadhamini zinapaswa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Bodi za Wadhamini Sura ya 318 (The Trustees’ Incorporation Act CAP 318), ili kuhakikisha usimamizi bora wa mali na rasilimali za taasisi wanazosimamia.

Kanyusi alieleza kuwa hadi kufikia Aprili 2026, jumla ya bodi za wadhamini 5,314 zimesajiliwa nchini, huku mikoa ya Ruvuma, Njombe, Mtwara na Lindi ikiwa na jumla ya bodi 321.

Hata hivyo, alikiri kuwepo kwa changamoto kadhaa, zikiwemo uelewa mdogo wa sheria, usimamizi usioridhisha wa mali na migogoro ya kiuongozi. “Changamoto hizi ndizo zilizotusukuma kuanzisha programu ya mafunzo kwa wadhamini kote nchini, ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na kanuni,” alisema.

Aliongeza kuwa RITA inaendelea kuboresha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na kufanya marekebisho ya sheria husika ili kuimarisha usimamizi wa bodi za wadhamini.

Mkutano huo ni sehemu ya chachu ya kuimarisha usimamizi wa bodi za wadhamini nchini, huku ukisisitiza misingi ya uwajibikaji, uwazi na ufanisi katika taasisi mbalimbali za umma na binafsi.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!