WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba, ametoa wito kwa jamii kuenzi maisha ya Polycarp Kardinali Pengo, kwa kuzingatia maadili, uaminifu na uzalendo aliyouishi wakati wa kipindi chake cha uongozi wa kiroho. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza 28 Februari 2026, kwenye ibada ya kuaga mwili wa Kardinali Pengo katika Kanisa la Hija Pugu, jijini Dar es Salaam, Jaji Warioba alisema, licha ya kutokuwa Mkatoliki, alimchukulia Kardinali Pengo kama kiongozi wake wa kiroho kutokana na msimamo wake thabiti katika kulinda maadili na ustawi wa jamii.
“Mimi si Mkatoliki, lakini nilimheshimu Kardinali Pengo kama kiongozi wangu wa kiroho. Alikuwa mtu anayezingatia sana maadili, uaminifu na uzalendo,” alifafanua Jaji Warioba.
Aidha, Jaji Warioba alikumbusha hotuba ya Kardinali Pengo wakati wa kuaga mwili wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akieleza kuwa ujumbe uliotolewa haukuwa mahsusi kwa familia au kwa waumini wa Kanisa Katoliki pekee, bali ulikuwa na maudhui mapana kwa Watanzania wote bila kujali imani zao.
“Ile hotuba aliyotoa haikuwa kwa familia tu, wala si kwa Wakatoliki pekee, ilikuwa kwa binadamu na Watanzania wote,” alieleza.
Kauli hiyo imeibua wito wa kutafakari mchango wa Kardinali Pengo katika kuimarisha mshikamano wa kitaifa na maadili ya jamii, huku viongozi na waumini wakimtaja kama kiongozi aliyesimama imara katika nyakati mbalimbali za kitaifa.
Aliyekuwa Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, aliyefariki 20 Februari 2026, anazikwa leo, ndani ya Kanisa la Bikira Maria, Pugu, jijini Dar es Salaam.
ZINAZOFANANA
Nchimbi akemea magomvi ya kivyama
Kardinali Pengo aagwa kanisani kwake
Makamu wa Pili wa Rais Z’bar, awaongoza wateja, wadau wa NBC kushiriki hafla ya futari