February 26, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NBC yakabidhi gari kwa Mshindi wa Kampeni ya Huduma za Kidigitali

 

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imekabidhi zawadi kuu za kampeni yake ya “Ukigusa Tu, iMOOO” kwa washindi wakubwa watatu wa kampeni hiyo ikiwemo zawadi kubwa ya gari aina Nissan X trail iliyokabidhiwa kwa Bw Salah Ahmed Mohamed mkazi wa jijini Dar es Salaam alieibuka mshindi wa zawadi kuu ya kampeni iliyolenga kukuza ujumuishaji wa kifedha kupitia uchocheaji wa matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya kidigitali

Hafla ya makabidhiano ya zawadi hiyo iliyohusisha pia makabidhiano ya zawadi kwa mshindi wa pili na watatu wa kampeni hiyo waliojishindia zawadi za simu janja aina ya Iphone 17 Pro na jiko la gesi na umeme imefanyika mapema leo, kwenye tawi la benki ya NBC tawi la Mlimani City, wilayani Ubungo jijini Dar es salaam ikiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya wateja Binafsi (wadogo na wakubwa) wa benki hiyo Bw Elibariki Masuke pamoja na maofisa wengine wa benki hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Masuke alisema kampeni hiyo haikulenga tu kutoa zawadi, bali ilibeba dhamira pana ya kijamii ya kuongeza uelewa na matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya kidigitali kwa makundi mbalimbali ya jamii.

Alieleza kuwa walengwa wa kampeni hiyo walijumuisha wafanyakazi, wafanyabiashara wadogo na wa kati, wanafunzi, pamoja na wateja binafsi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha na kupunguza changamoto za miamala ya ana kwa ana.

“Katika dunia ya leo, huduma za kifedha kidigitali si anasa tena, bali ni nyenzo muhimu ya kurahisisha maisha ya kila siku. Kupitia kampeni hii, tumeshuhudia ongezeko la matumizi ya kadi, mashine za POS na programu tumizi ya NBC Kiganjani, jambo linaloashiria mwamko chanya wa jamii kuelekea uchumi wa kidigitali,” alisema Bw. Masuke.

Aliongeza kuwa mbali na washindi wakuu watatu waliokabidhiwa zawadi zao leo, benki hiyo imekuwa ikitoa zawadi za kila wiki kwa washindi wengine wengi, zikiwemo fedha taslimu na kompyuta mpakato, kama sehemu ya kuhamasisha tabia ya kuweka akiba, kufanya miamala salama na kutumia teknolojia kwa maendeleo binafsi na ya biashara.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Idara ya Miamala wa NBC, Bw Mangire Kibanda alisema kupitia kampeni hiyo, NBC imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuchangia ajenda ya kitaifa ya ujumuishaji wa kifedha na ujenzi wa jamii inayotumia teknolojia kwa maendeleo.

“Benki tutaendelea kubuni programu na kampeni zenye kugusa maisha ya Watanzania, kwa kuzingatia mahitaji halisi ya jamii na mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea duniani.’’ aliongeza

Akizungumza kwa niaba ya washindi wote wa kampeni hiyo Bi. Diana Bernard aliyemwakilisha mshindi wa zawadi kuu, aliishukuru NBC kwa kuandaa kampeni yenye tija kwa wateja na jamii kwa ujumla. Alisema wao kama familia wamekuwa wateja wa muda mrefu wa benki hiyo kutokana na ubora wa huduma na urahisi wa matumizi ya mifumo ya kidigitali.

“Zawadi hii si tu gari, bali ni ushuhuda wa namna taasisi za kifedha zinavyoweza kubadilisha maisha ya watu kwa kuwapa motisha ya kutumia huduma rasmi za kifedha. Huduma za kidigitali zimetusaidia kuendesha shughuli zetu binafsi na biashara kwa ufanisi mkubwa. Tunajivunia kuwa sehemu ya mabadiliko haya,” alisema.

Mbali na zawadi ya gari, washindi wengine waliokabidhiwa zawadi zao ni Bi. Bw. Vidya Sagar aliyejishindia simu janja aina ya iPhone 17 Pro pamoja na Beatrice Chengula wa Temeke aliyejishindia jiko la gesi na umeme.

About The Author

error: Content is protected !!