February 24, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Kesi ya Lissu yasimama, Serikali yakimbilia Mahakama ya Rufaa

Tundu Lissu akiwa mahakamani

 

KESI ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demkrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu imeendelea kuwa kaa la moto, baada ya serikali kukimbilia mahakama ya rufaa kupigania ushahidi uliokataliwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hatua hiyo ya serikali ilitokana na uamuzi wa Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, kukataa ushahidi wa nyongeza ulioombwa na upande wa Jamuhuri na kupingwa na mshatakiwa.

Uamuzi huo uliotolewa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akishirikiana na Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde uliotokana na notisi ya Jamhuri ya kutaka kuwasilisha nyongeza ya ushahidi kwenye ushahidi wa ACP Aman Mahamba.

Kutokana na hatua hiyo ya mahakama, upande wa Jamhuri umesilisha notisi nyingine katika Mahakama ya Rufaa kutaka mahakama hiyo kufanya marejeo ya uamuzi wa Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, uliokataa ushahidi wa nyongeza kwenye kesi Na. 19605/2025 ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu.

Wakili wa Serikali Mwandamizi Renatus Mkude amedai mahakamani hapo kuwa kifungu cha 6 cha Appellate Jurisdiction Act na kanuni ya 65(1) ya kanuni za Mahakama ya Rufani.

Wakili Mkude amedai kuwa notisi hiyo imepokelewa katika mahakama ya rufaa kwa mifumo ya kielektroniki inayotambulika na Mahakama na kusajili kama mapitio ya jinai) Na. 7203216/2026 imepokelewa na Mahakama ya Rufani Tanzania.

Upande wa serikali umetanabaisha kuwa lengo lao mahakama ya rufani ifanye mapitio ya uamuzi wa mahakama kuu.

“Jopo la Majaji wa Mahakama Kuu, kwa kuwa shahidi wetu aliyekuwa akifuata ACP Mahamba tulimuombea notisi husika ya ushahidi wa nyongeza na uamuzi wa mahakama haukuwa upande wa mashtaka, hiyo ndiyo sababu ya kuomba marejeo haya,” alieleza Mkude.

Aliongeza “Ni rai yetu kwa kuwa shauri limeshapokelewa Mahakama ya Rufaa na kupewa namba, tunaomba kusimama ili kutoa nafasi ya kusikilizwa kwa rufani hiyo.”

Baada ya maelezo hayo, Lissu aliomba apewe nakala ya wasilisho la Jamhuri walilolipeleka Mahakama ya Rufaa.

Aidha, alidai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 8(2)(d), hakiruhusiwi kukata rufaa, kuomba mapitio au marejeo dhidi ya uamuzi wa mahakama ambao haujahitimisha kesi.

“Mnataka mnipeleke huko ili huku kesi isimame niendelee kukaa gerezani. Nataka niwaambie Majaji kwamba nitawafuata huko huko na nitawashughulikia,” alieleza Lissu.

Mbali na hilo, Lissu alilalamikia kukosa haki ya mawasiliano ya faragha na wanaomtembelea gerezani, wakiwemo mawakili wake.

Akitoa mwelekeo wa mahakama, Jaji Dunstan Ndunguru alisema, “Shauri linasimama hadi Mahakama ya Rufaa itakapotoa uamuzi.”

Hivyo, mwenendo wa kesi hiyo sasa utategemea uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kuhusu maombi ya mapitio yaliyowasilishwa na Jamhuri, baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali notisi ya ushahidi wa nyongeza.

About The Author

error: Content is protected !!