BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana kwa ukaribu na wadau mbalimbali wakiwemo Serikali, wafanyabiashara, wawekezaji, wajasiriamali, wafanyakazi, wakulima pamoja na makundi mengine ya kijamii, kwa lengo la kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia utoaji wa huduma jumuishi na bunifu za kifedha zinazoendana na mahitaji halisi ya makundi ya kiuchumi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Tanga … (endelea).
Hatua hiyo inalenga kuunga mkono jitihada za Serikali katika kujenga uchumi shindani na jumuishi, kwa kuhakikisha wananchi na taasisi mbalimbali wanapata huduma bora, nafuu na rafiki za kifedha zitakazowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo.
Dhamira hiyo ilisisitizwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, mbele ya Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula (Mb), wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea banda la maonesho ya benki hiyo katika Viwanja vya Usagara, mkoani Tanga, kunakofanyika Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa. NBC ni miongoni mwa wadhamini muhimu wa maadhimisho hayo yaliyozinduliwa rasmi na Naibu Waziri huyo.

Akizungumza katika maonesho hayo, Sabi alisema NBC imeendelea kubuni na kuboresha huduma zake ili kukidhi mahitaji ya makundi mbalimbali, ikiwemo huduma za ndogo na kubwa, mikopo kwa wajasiriamali, mikopo ya kilimo, biashara na viwanda, pamoja na huduma za kifedha kwa taasisi na miradi mikubwa ya kimkakati ya maendeleo.
“Tunatambua kuwa ukuaji wa uchumi unahitaji mifumo imara ya kifedha. Ndiyo maana NBC tumejikita katika kutoa suluhisho rafiki za kifedha kupitia huduma za kidijitali, mikopo yenye masharti nafuu, pamoja na ushauri wa kitaalamu kwa wateja wetu ili waweze kukuza biashara na uzalishaji wao,” alisema Sabi.
Aliongeza kuwa benki hiyo imeendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa za kifedha (FinTech) ili kuongeza upatikanaji wa huduma hata kwa wananchi walioko maeneo ya vijijini, sambamba na kuimarisha ushirikiano na Serikali katika utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula, aliwapongeza na kuzishukuru taasisi za kifedha ikiwemo benki ya NBC kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha sekta ya fedha nchini na kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza uchumi jumuishi.
“Serikali inaendelea kuhimiza taasisi za kifedha, kuja na bidhaa na huduma zitakazowagusa wananchi moja kwa moja. Tunashukuru kuona taasisi hizi zimewekeza zaidi jitihada zao katika katika huduma za kidijitali, mikopo kwa sekta za uzalishaji na kushirikiana na wadau mbalimbali katika maendeleo ya uchumi,” alisema Bw. Luswetula.
Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa taasisi za kifedha ili ziweze kuchangia ipasavyo katika kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya wananchi, huku akihimiza wananchi kutumia fursa za huduma za kifedha zinazotolewa na benki mbalimbali ikiwemo NBC.

Kwa upande wake, Meneja wa NBC Mkoa wa Tanga, Moses Charles alisema benki hiyo imejipanga kikamilifu kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa huo kwa kuzingatia fursa za kiuchumi zilizopo ikiwemo kilimo, biashara, viwanda vidogo na vya kati, pamoja na uwekezaji katika sekta ya bandari na usafirishaji.
Alisema mkakati wa NBC mkoani Tanga umejikita katika kuwawezesha wakulima na wajasiriamali kupitia mikopo maalum, huduma za kidijitali zitakazorahisisha miamala, pamoja na kutoa elimu ya kifedha kwa wananchi ili kuongeza uelewa na matumizi sahihi ya huduma za benki.
“Tunaamini Tanga ina nafasi kubwa ya kukua kiuchumi. Kupitia huduma zetu za kifedha, tunalenga kuwa mshirika wa karibu wa wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji wa mkoa huu katika kufanikisha miradi yao na kuongeza ajira,” alisema Meneja huyo.
ZINAZOFANANA
Kindege cha Aviator kutoka Meridianbet kuleta zawadi ya Samsung A26
Tundu Lissu asherehekea Birthday gerezani
Kalamba Games kuja na burudani mpya isiyo kikomo ndani ya Meridianbet