January 14, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mvutano wa kisheria wagubika Mahkama ya Z’bar

Mwanasheria Mkuu wa ACT Wazalendo, Omar Said Shaaban

 

JOPO la Mawakili wanaomwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeishikilia hoja ya kutaka Mahkama Kuu ya Zanzibar itambulike kuwa haina mamlaka wala uwezo wa kisheria wa kusikiliza mashauri yanayohusu uchaguzi wa ubunge upande wa Zanzibar. Anaritpoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Mbele ya Jaji Haji Suleiman Khamis, mawakili hao wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Alan Shija, waliieleza Mahkama Kuu inayoketi Tunguu nje ya mjini Zanzibar, kuwa hoja yao inazingatia muongozo unaotolewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Akitoa maelezo ya kukazia hoja yao, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nalindwa Sekimanga, alieleza kuwa Ibara ya 83{1} ya Katiba hiyo na vifungu vyake {a} na {b}, vinatamka wazi kuwa masuala yanayohusu uteuzi na uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano yatashughulikiwa na Mahkama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakili wa Serikali Mwandamizi Nalindwa akataja kwa yeyote mwenye kuhitaji kulalamika kuhusu uchaguzi wa ubunge, kama walivyoomba walalamikaji walioko Zanzibar, anawajibika kisheria kufuata maelekezo hayo kwa kufungua shauri mbele ya mahkama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania si vinginevyo.

Anaeleza kuwa pamoja na ukweli kuwa katiba hiyo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua kuwepo Mahkama Kuu ya Zanzibar, haijaitaja au kuipa mamlaka ya kushughulikia jambo lolote linalohusu malalamiko dhidi ya uchaguzi wa wabunge.

Hoja hii iliibuliwa kwa mara ya kwanza mahkamani hapo tarehe 6 Januari mwaka huu, pale kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi wa wabunge katika majimbo 19 ya Unguja zilitajwa, baada ya uamuzi mdogo aloutoa Jaji Haji kufuatia hoja ya awali ya upande wa walalamikaji iliyotaka wanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wasiruhusiwe kumwakilisha mwanasheria mkuu wa SMT katika kesi hizo.

Baada ya uamuzi huo, uliotokana na hoja zilizotolewa na Wakili Omar kwamba wanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa SMZ wasitambuliwe kuwa mawakili wa walalamikiwa, ndipo upande wa Jamhuri ulipoibua rasmi hoja ya kuhoji mamlaka ya mahkama ya Zanzibar na kutaka mahkama iamue kwanza ndipo usikilizaji uanze.

“Upande wetu {walalamikiwa} tunashikilia kuwa Mahkama Kuu ya Zanzibar haina mamlaka na uwezo kusikiliza mashauri haya ya uchaguzi wa wabunge. Tunahimiza mamlaka yatafutwe kwenye sheria na sio kwa tafsiri. Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaelekeza wapi pafuatwe ili kulalamika; haiwezi kuwa zikafunguliwa na kusikilizwa mbele ya Mahkama hii,” hitimisho la hoja upande wa Mwanasheria Mkuu wa Muungano.

Mlalamikiwa namba moja kwenye kesi hizo ni Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania {INEC} ya mwaka 2024 ambayo ndiyo inayoendesha na kusimamia uchaguzi huo wa Rais wa Tanzania, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Madiwani wa Tanzania Bara.

Wakili Omar anawakilisha walalamikaji kwenye majimbo 19 ya kisiwani Unguja wanaotaka matokeo ya uchaguzi uliofanyika tarehe 29 Oktoba 2025 yatamkwe kuwa si ya halali na yatenguliwe. Kesi nyengine 14 zilizofunguliwa mahkama hiyohiyo ya Zanzibar kisiwani Pemba, ziliunganishwa jana pale Jaji Haji aliporidhia kuwa ni busara na kuhifadhi muda wa mahkama kuruhusu zisikilizwe pamoja na zilizopo Unguja.

Akijibu hoja za upande wa Jamhuri leo, Wakili Omar alieleza kuwa anahofia kuwa wanasheria wenzake wamechukua tafsiri isiyo sahihi wanavotaja Ibara ya 83 ya Katiba ya Muungano. Anadai kuwa ni muhimu kwanza kuisaidia mahkama kuelewa maana ya hiyo tafsiri iliyofanywa na wanasheria wa upande wa walalamikiwa, na mahkama ijue hayo mamlaka yanayobishaniwa yanatokana na nini hasa.

Akataja kuwa maelezo murua kuhusiana na suala hilo yapo kwenye jarida la kisheria la England, Toleo la Nne, Fungu la Kumi, aya ya 314. Tafsiri hiyo imekutwa wakati wa kuamua rufaa iliyomhusu Paul John Muhozya dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Muungano.

Alidai ni msimamo wake kuwa suala la mamlaka ya mahkama kuu ya Zanzibar halitokani na fadhila ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bali Katiba ya Zanzibar ambayo inaitambua na kuipa mamlaka yasiyo na mipaka na wajibu wa kusikiliza mashauri ya aina yoyote – ya jinai na mengineyo.

Kifungu cha 93 kinaitambua Mahkama Kuu ya Zanzibar kuwa yenye mamlaka ya kutoa maamuzi yanayofaa kuwa kumbukumbu. Alidai kuwa kifungu tatu kinaeleza mamlaka hayo yataendelea kuwepo na kwa hivyo yatakuwa yasiyo na mipaka kusikiliza na kuamua jambo lolote la kisheria lililowasilishwa kwa mujibu wa sheria inayotumika Zanzibar.

Akiitumia Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Namba Moja ya mwaka 2024, pamoja na Kanuni za Uchaguzi kwa ajili hiyo, Wakili Omar alieleza sheria imesema wazi kuwa itatumika Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar isipokuwa tu kwa kesi zinazohusu udiwani ambazo zitafunguliwa na kusikilizwa mahkamani Tanzania Bara pekee.

Wakili huyo alijenga hoja pia kuzingatia alichodai kwenye suala muhimu la uwajibikaji kunahitajika pia kuwepo mkazo wa utambuzi wa haki ya wananchi kupata haki wanapokuwa na malalamiko, na kwamba “unamsaidia vipi mwananchi kuifikia haki kwa yule aliyeko Micheweni kumtaka akafungue kesi Sumbawanga, au Dar es Salaam, au Dodoma?”

Kwa upande wake, naye alishikilia kuwa nguvu ya Ibara 115 na 83 zote zinaitambua mahkama kuu ya Zanzibar na kwa hivyo, anaiomba Mahkama iliyoko mbele ya Jaji Haji, itupilie mbali pingamizi linalohoji mamlaka ya Mahkama ya Zanzibar kusikiliza kesi za uchaguzi wa wabunge.

Jaji Haji aliakhirisha kesi akisema tarehe 27 Januari 2026 atakuja kutoa uamuzi mdogo wa pingamizi hilo. Siku inayofuata, tarehe 28 Januari, alishapanga kuwa zitakuja kusikilizwa kesi hizo ikianzia na ombi la walalamikaji kuondolewa gharama za dhamana ya ufunguaji wa kesi hizo.

About The Author

error: Content is protected !!