January 13, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Hatuwezi kuongeza maslahi ya majaji kwa sasa – Samia

Rais Samia Suluhu Hassan

 

RAIS wa Jamhuri, Samia Suluhu Hassan, amemtaka Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju, kujipima maslahi wanayopata majaji na madaktari nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Samia alitoa kauli hiyo, leo Jumanne, tarehe 13 Januari, mjini Dodoma, wakati akihutubia mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA).

Alikuwa akijibu kauli ya Jaji Masaju, aliyetaka kuboresha maslahi ya majaji na mahakimu nchini.

Alisema, “Jipime wewe na mtu ambaye afya yako ikiteteleka anakwenda kukutengeneza. Kule anakurudishia afya yako na hali yako uwe jaji bora, lakini bado mazingira yake ya kazi ni magumu na stahili zake ni ndogo sana. Tujipime hapa.”

Akaongeza, “Nataka niwaibie siri hapa, napata barua za maombi ya kuboresha maslahi, naambiwa kama walivyo majaji na sisi tunataka tuwe hivyo.

“Kwa hiyo, wakati wewe unalia pete yako uliyovaa sio nzuri, mwenzao analia hata kidole cha kuvalia hiyo pete hana; na hata pete mbaya hana.”

Kwa mujibu wake, serikali haina uwezo wa kufanya kila kitu, kana kwamba tunaishi kwenye ulimwengu wa mawazo ya kufikirika.

“Tanzania hii inauwezo wa kila kitu…twendeni polepole. Maendeleo ni hatua, tumeanza hatua za awali na nyie mmeona tumechukua hatua kubwa za kuijengea heshima kubwa mahakama,” alifafanua.

Samia amesema, amepokea barua kutoka kwa watumishi mbalimbali wa umma wenye kuimba serikali kuongozewa maslahi yafanane na yale ya mahakimu na majaji.

Mapema Jaji Masaju, alimuomba kuongeza bajeti ya Mahakama na kuboresha maslahi ya watumishi wa mahakama kwa ujumla.

Miongoni mwa maslahi hayo, ni kuimarisha huduma ya bima ya afya ili ziendene na mahitaji na asili ya kazi wanazofanya.

Hata hivyo, Rais Samia amesema, hatayapuuza maombi hayo na kuongeza kuwa “Nikisema hivyo sisemi kwamba hatutaangalia maslahi yenu twendeni. Hapana. Twendeni polepole.”

About The Author

error: Content is protected !!