September 19, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Askofu Shoo kubadili Katiba, kubaki madarakani?

 

DK. Frederick Shoo, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini yenye makao yake mjini Moshi, “huenda akabadili Katiba,” ili kuendelea kubaki madarakani. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Taarifa kutoka Moshi na Arusha zinasema, kuna uwezekano mkubwa wa Askofu Dk. Shoo, mkuu wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini, “akabadili Katiba,” ili kuendelea kuhudumu kwenye wadhifa huo, kinyume na Katiba ya dayosisi yake na ya KKKT.

Kwa mujibu wa katiba ya Dayosisi ya Kaskazini na Katiba ya KKKT, kiongozi wa dayosisi hiyo, anapaswa kuhudumu kwa muda usiozidi miaka kumi. Askofu Shoo ameishapitisha umri wa kustaafu wa miaka 65.

Madai kuwa Askofu Dk. Shoo anaweza kubadili Katiba ya kanisa lake, yameibuliwa na makundi mbalimbali.

Kundi la kwanza ni jimbo la Masama lililoko Hai ambalo limetoa nyaraka mbili mfululizo zinazomtuhumu Askofu Shoo kwa upendeleo, ukabila, ubadhilifu wa mali, dharau na kuchezea katiba ya dayosisi. Kundi hilo limemuonya asijaribu kuongeza muda wa kukaa ofisini.

Nao wanaojiita, “waumini wa Kilutheri na mashahidi wa Kanisa,” katika andishi lao kwa maaskofu wa kanisa hilo la pili kwa ukubwa nchini, tarehe 15 Agosti 2024.

Katika andishi hilo, ambalo tumepata nakala yake, waumini wanawaeleza maaskofu hao kuwa “…juma lililopita, tuliweka mbele yenu tuhuma zenye ukweli kuhusu Askofu Shoo kuvuruga Dayosisi yake kwa kuandaa mpango ili aongezewe muda baada ya kukosa ukuu wa KKKT.

“Pia tuliweka wazi uhusiano wake na … (jina tunalihifadhi) aliyetumika kuvuruga Dayosisi ya Mwanza. Juma hili, amevamia semina ya wanahabari wa KKKT iliyofanyika Dar es Salaam. Semina ilikuwa ameandaliwa ili kupiga debe mradi wa Katiba moja. Bahati nzuri Mungu akaepusha hila hiyo kwa kuchelewesha fedha” kufika kwenye makao makuu ya kanisa.

Mkutano mkuu wa 38 wa Dayosisi ya Kaskazini, unatarajiwa kufanyika tarehe 30 Agosti mwaka huu.

Aidha, taarifa kuwa Askofu Dk. Shoo kutaka kubadili Katiba ili kuendelea kubaki madarakani, kumetajwa pia na maaskofu watatu wastaafu – Isaya Mengele, Job Mbwilo na Hance Mwakabana – katika barua yao kwa mkuu wa kanisa hilo, Askofu Dk. Alex Malasusa na maaskofu walioko madarakani.

Maaskofu hao watatu, wanasisitiza kwamba tuhuma zinazomkabili Askofu Shoo, “haziwezi kupuuzwa.”

Miongoni mwa wanayotaja, ni madai ya ukosefu wa maadili; mkakati wa kutaka kujiongezea muda zaidi ili aendelee kuwa askofu wa Dayosisi yake hata baada ya kufikisha umri wa kustaafu na matumizi mabaya ya mali ya Kanisa.

Tuhuma nyingine, ni “usababishaji wa migogoro katika maeneo mbalimbali kwa manufaa yake binafsi, chuki binafsi dhidi ya maaskofu wenzake, hasa waliokuwa na ujasiri wa kumkosoa na kumsahihisha kwa mambo yake yasiyokubalika.

Aidha, maaskofu wanamtuhumu kiongozi wao huyo wa zamani, “kutoheshimu hadhi ya Baraza la Maaskofu na hivyo kulifanya lisiweze kutimiza wajibu wake kama inavyostahili, pamoja na upendeleo usiofaa na uliopitiliza mipaka, kwa manufaa binafsi.”

Barua ya maaskofu hao watatu, yenye takribani kurasa saba, imenakiliwa kwa maaskofu wote walioko kazini na imebeba kichwa cha maneno kisemacho: “Mtazamo, Maoni na Ushauri Wetu.”

wanaHALISI Online limeshindwa kumpata Askofu Dk. Shoo, kufafanha madai hayo. Linaendelea kumtafuta.

About The Author