Mvua kubwa
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mifumo ya hali ya hewa iliyopo kwa sasa inaonesha kuendelea kuimarika kwa ukanda wa mvua, hali inayosababisha kuendelea kushuhudiwa kwa vipindi vya mvua kubwa katika baadhi ya mikoa nchini. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA, mikoa inayotarajiwa kupata mvua kubwa 29 Desemba mwaka huu ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Mara, Simiyu, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Morogoro, Ruvuma, Lindi na Mtwara.
TMA imesema hadi sasa imepokea taarifa zinazoonesha mvua hizo zimesababisha athari katika miundombinu mbalimbali, ikiwemo reli ya zamani ya MGR baada ya madajara kuathirika katika eneo la Kidete wilayani Kilosa mkoani Morogoro na eneo la Gulwe wilayani Dodoma. Athari nyingine ni hitilafu za umeme wa TANESCO pamoja na umeme wa reli ya kisasa ya SGR.
Aidha, barabara kuu ya Morogoro–Iringa katika eneo la Mama Marashi–Mikumi imeripotiwa kukumbwa na maporomoko ya mawe na mrundikano wa tope barabarani, hali iliyoathiri usafiri wa abiria na shehena kwa ujumla, hususan kupitia reli ya SGR.
Kutokana na hali hiyo, TMA imewashauri wananchi kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa pamoja na kufuata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.
Vilevile, TMA imesema itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa nchini na kutoa taarifa mara kwa mara kadri inavyohitajika.
ZINAZOFANANA
TRC yaomba radhi na kuongeza safari za SGR
Mwigulu akagua uzalishaji na usambazaji maji Ruvu chini
Dk. Mohamed aendeleza mageuzi katika jamii ya Mtambwe