MAMLAKA ya hali ya hewa Tanzania (TMA), imetoa tahadhari ya kuwapo mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa 20 nchini. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo, leo Jumamosi 27 Desemba 2025, mikoa iliyohatarini kukumbwa na mvua, ni pamoja na Arusha, Kilimanjaro na Manyara.
Mikoa mingine itakayokabiliwa na hali hiyo, ni Kigoma, Katavi, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Morogoro, Ruvuma, Tanga, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara na Pwani.
TMA imesema mvua hizo zinatarajiwa kunyesha Jumapili, tarehe 28 Desemba 2025 na huenda zikasababisha madhara mbalimbali ikiwamo mafuriko, maporomoko ya udongo na usumbufu wa shughuli za kiuchumi na kijamii.
Mamlaka imewataka wananchi wanaoishi katika maeneo yaliyotajwa, hususan walioko mabondeni na maeneo hatarishi, kuchukua tahadhari za mapema ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.
Katika hatua nyingine, TMA imewataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa na utabiri wa hali ya hewa unaotolewa mara kwa mara, ili kupata taarifa sahihi na kwa wakati.
Januari mwaka jana, mvua kubwa zilizonyesha nchini Tanzania, zilisababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali, ikiwamo jiji la Dar es Salaam.
Mafuriko hayo, yalileta maafa kutokana na kuharibika kwa miundo mbinu na mji kugawanyika mara mbili kufuatia na kukatika kwa madaraja.
Jumamosi alfajiri tarehe 20 Januari 2024 watu kadhaa waliripotiwa kufariki, nyumba kadhaa zilizoko karibu na mto zilianguka na barabara zikiharibiwa baada ya mvua kubwa kunyesha kwa muda wa siku mbili.
Kwa mfano, katika eneo la Kunduchi, huko Tegeta, barabara na madaraja yaliharibika, hatua ambayo ilifanya kuwa vigumu kwa watu kusafiri kutoka sehemu moja kwenye nyingine.
Aidha, mwaka 2023 mvua kubwa iliathiri maeneo ya kaskazini mwa Tanzania tangu Oktoba wakati wa msimu wa mvua za Oktoba na Desemba na kusababisha mafuriko, mito kujaa na maporomoko ya ardhi.
Mnamo tarehe 2 Desemba 2023, maporomoka ya ardhi yalitokea katika kijiji cha Kateshi katika Wilaya ya Hanang Magharibi mwa Manyara, na kusababisha uharibifu mkubwa ulioripotiwa.
Maporomoko hayo pia yaliharibu miundombinu ya umma, ikiwemo barabara, umeme, na mifumo ya mawasiliano na maji.
Haijaweza kufahamika mvua za mwaka huu, zitakuwa na uharibifu wa kiwango gani.
ZINAZOFANANA
Watumishi TEMESA wafutwe kazi – Mwigulu
BAKWATA yapigwa mweleka mahakamani
Meridiansport yaikumbuka jamii, yatoa msaada faraja Care Orphanage Centre