December 6, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

TRA yawataka wanachama wa SACCOS kuhamasisha ulipaji kodi

 

KAMISHNA wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, amewataka wanachama wa Saccos nchini kuwa mabalozi wa kuhamasisha wananchi kulipa kodi na kutumia mikopo kuanzisha shughuli za kiuchumi zitakazoongeza wigo wa walipa kodi nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Amesema, lengo la saccos za watumishi wa umma ni kuwawezesha kiuchumi ili kuongeza ustawi wa kaya na kuhakikisha watumishi wanatimiza majukumu yao kwa uadilifu bila vishawishi vya rushwa.

Mwenda, ambaye pia ni Mlezi wa TRA Saccos, amesema hayo leo tarehe 6 Desemba 2025 jijini Dar es Salaam katika Mkutano Mkuu wa 20 wa mwaka 2025 ulioandaliwa na TRA Saccos wenye kauli mbiu “Miaka 20 ya kuinua uchumi wa mwanachama wa mwanachama kupitia huduma bora na ubunifu”.

“Kama tunataka kujenga uchumi wa kila mtu mmoja mmoja na baadaye uchumi wa taifa, lazima tuhamasishe matumizi sahihi ya mikopo. Mkopo ukitumika kununua TV hautoi mchango wowote katika kuongeza walipa kodi lakini ukitumika kuanzisha biashara, taifa linapata kodi na kijana anapata ajira,” amesema Mwenda.

Amesema bado idadi ya wanachama ni ndogo ukilinganisha na watumishi wote wa TRA, hivyo akasisitiza juhudi za kuwafikia na kuwashawishi watumishi zaidi kujiunga ili wanufaike na mikopo yenye riba nafuu.

Aidha, aliwasihi wanachama wote kulinda amani na uchumi wa taifa kwa kuepuka kushiriki au kuunga mkono vitendo vinavyosababisha vurugu na uharibifu wa mali za umma, akitoa pole kwa waliopoteza ndugu au kuumia katika matukio ya vurugu za karibuni.

Kwa upande wake, Naibu Mrajis Mkuu wa vyama vya ushirika wa kifedha CPA Josephat Kisamalala, amesema Saccos imefanikiwa kutoa ajira 10,000 kwa wananchi kwa mwaka 2024, hivyo kuifanya Tanzania kushika nafasi ya tano kwa ubora wa Saccos duniani.

“Kupitia mafanikio haya kumeifanya TRA Saccos kushika nafasi ya tatu na zaidi ya bilioni 90 zimekusanywa kama akiba mwaka 2023, hivyo kuendelea kuchangia pato la taifa na hiyo yote ni kutokana na mazingira mazuri kutoka kwa mwajiri na shauri endeleeni kulinda jina la mwajiri,” amesema Kisamalala.

Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa taarifa ya Baraza la Saccos Duniani, Tanzania inashika nafasi ya tano, ikizidiwa na Kenya, Ghana, Ethiopia na Cameroon. “Tunatarajia katika taarifa ijayo Tanzania iwe nafasi ya kwanza na hilo linawezekana,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TRA Saccos, Mbogo Kerege, amesema wanatarajia kujenga jengo lao litakalowasaidia kufanya shughuli zao pamoja na kufungua fungamanisho la pamoja litakaloruhusu mwenza wa mwanachama na watoto kuwa wanachama waweze kupata mikopo na kuwaepusha wanachama na mikopo ya kausha damu.

About The Author

error: Content is protected !!