MAKAMU wa Rais, Balozi Emmanuel Nchimbi, amesema ukarabati wa reli ya TAZARA utaimarisha ukanda wa kati na kusini, kuchochea biashara kati ya Tanzania, Zambia; Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Bara la Afrika kwa ujumla. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zambia … (endelea).
Amesema, “…ukarabati huu, utaongeza mauzo ya bidhaa nje na ndani ya mataifa ya Zambia na Tanzania, kukuza kilimo, madini, viwanda, utalii na kutengeza ajira zaidi kwa wananchi.”
Balozi Nchimbi, ametoa kauli hiyo, katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la uzinduzi wa ukarabati wa Reli hiyo, iliyofanyika Lusaka, Zambia.
Amesema wakati reli ya TAZARA inaimarishwa, Tanzania inafanya maboresho ya kisasa ya bandari ikiwemo upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam kwa magati mapya, kuboresha ufanisi na kuhakikisha muunganiko mzuri wa Reli ya Umeme ya Kisasa (SGR) na TAZARA.
Amesema, Tanzania itaendelea kuziboresha bandari zake za Tanga, Mtwara na Bagamoyo, ili kuhakikisha kunakuwa na ubora wa kimataifa wa usafirishaji kwa nchi za Zambia, SADC na Afrika kwa ujumla.
Ukarabati huo, unafadhiliwa na serikali ya China na kuongeza kwamba historia inafundisha ukweli wenye nguvu kwamba, Tanzania, Zambia na China zinaposimama pamoja, hakuna changamoto iliyo kubwa sana.
Aidha, kiongozi huyo amesema, ukarabati huo unakuja wakati China inaibuka kama mdau muhimu wa ukuaji wa uchumi kimataifa chini ya mpango wake wa 15 wa miaka mitano.
Amesema hali hiyo inaiweka China kama mshirika muhimu wa maendeleo.
Mamlaka ya Reli ya Tanzania–Zambia (TAZARA), ni miongoni mwa alama muhimu za urafiki na ushirikiano kati ya Serikali za Tanzania, Zambia na Jamhuri ya Watu wa China.
Amesema, ikiwa waasisi wa mataifa hayo, waliweza kujenga Reli ya Uhuru, kwa sasa ikizingatiwa mataifa na uwezo yaliyonayo yataweza kukarabati Reli ya TAZARA na kuifanya kuwa mfano wa ushirikiano wa karne ya 21.
Reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,860 ikiwa na kilomita 975 kwa Tanzania na kilomita 885 nchini Zambia, inaunganisha Bandari ya Dar es Salaam na Kapiri-Mposhi Mpya, kwa kutumia mfumo wa Cape Gauge (milimita 1,067).
Ukarabati huo utafanywa kwa njia ya reli, stesheni, mifumo ya mawasiliano, pamoja na ununuzi wa treni 34, mabehewa 760, makochi 18 na treni 2 kwa ajili ya huduma za abiria.
Ufufuaji huo unalenga kuongeza usafirishaji wa mizigo hadi kufikia tani 2.4 milioni ifikapo mwaka wa tatu wa uendeshaji.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Zambia, Hakainde Hichilema pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China, Li Qiang.
Balozi Nchimbi ameambatana na Katibu Mkuu wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara; Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Luteni Jenerali Mathew Mkingule; Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Machibya Masanja na Mkurugenzi Mkuu TASAC Mohamed Salum.
ZINAZOFANANA
Serikali yaanza kuonja kibano cha kimataifa
Mtanzania aliyeuawa Israel azikwa
Zitto Kabwe azinduka usingizini