ASKOFU Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amesema, hata kama makanisa yake yatafungiwa milele, lakini hayuko tayari kunyamazia vitendo vya utekaji na watu kupotezwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza leo Jumapili, kupitia mitandao ya kijamii, Gwajima amevikumbusha vyombo vya dola, umuhimu wa kuwasaka “magenge ya watu, yanayojihusha na vitendo hivyo.”
“Wajibu wa vyombo vya dola, ni kulinda rai ana kulinda viongozi waliopo kwa mujibu wa Katiba. Siyo sahihi kwa vyombo hivyo, kunyamazia matendo haya kana kwamba hawahusiki nayo,” ameeleza.
Amesema, kuna ushahidi wa kutosha wa watu kutekwa, uliotolewa na baadhi ya waliopatwa na mkasa huo.
Miongoni mwao, amemtaja Edgar Mwakalebela, maarufu kwa jina la Sativa, aliyetekwa tarehe 23 Juni mwaka jana na kutelekezwa kwenye msitu huko Katavi, mkoani Rukwa.
Kwa mujibu wa Gwajima, hata waliomteka Polepole, wanafahamika kwa kuwa baadhi ya watekaji husimulia waliyotenda baada ya kukamilisha kazi yao.
Kauli ya Gwajima imekuja wakati baadhi ya viongozi wa madhehebu ya kidini nchini, wanasiasa, viongozi wa vyombo vya dola, serikali na watu wengine mbalimbali, wakitoa wito kwa wananchi, kudumia amani na utulivu wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.
Katika hotuba yake hiyo, Askofu Gwajima amesema, suala la utekaji halikubaliki hata kidogo, na kwamba yeye binafsi, ameanza kupaza sauti tokea alipotekwa Mohammed Dewji ‘Mo Dewji,’ kipindi cha utawala wa Rais John Magufuli.
Akizungumza kwa uchungu, Gwajima anasema, alipotekwa Mohammed Dewji, alipiga kelele na kuwataka waliomteka kumrudisha mara moja.
Mbunge huyo wa zamani wa jimbo la Kawe, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameendelea kusisitiza kuwa sauti yake ya sasa, kuhusu masuala ya utekaji na watu kupotea, haitokani na utawala uliyopo.
Ameongeza, “Roma na Mo Dewji walipotekwa nilipaza sauti tena ilikuwa kipindi cha Magufuli. Mtu akifanya mambo mema anatakiwa asifiwe, lakini akifanya maovu akemewe.”
Akaongeza, “Utekaji hauna dini. Hauna muislamu wala mkiristo,” na kwamba nchi hii si mali ya mtu binafsi au taasisi moja.
Kwa maoni yake, anaamini kuwa kuna kikundi cha watu kinashughulika na masuala ya utekaji na sio vyombo vya dola.
“Ndio maana mimi nasema kuna kakikundi kimashughulika na masuala ya utekaji na ninapoongelea kakikundi hako, kuna watu wanakasilika,” ameeleza.
Amewataka wananchi kuamka na kukemea masuala ya utekaji, huku akisisitiza kuwa jambo linaweza kutokea kwa jirani yako linaweza kutokea kwenye nyumba yako.
“Ili haya masuala ya utekaji yaishe, lazima vyombo vya ulinzi na usalama vijitenge,” ameeleza.
Akihutubia Bunge la Jamhuri, tarehe 27 Juni 2025, Rais Samia Suluhu Hassan, aliliagiza jeshi la Polisi nchini, kuchunguza matukio ya utekaji.
ZINAZOFANANA
Chadema yataka Heche achiwe huru
Mahakama: Hakuna ushahidi Polepole anashikiliwa na IGP na wenzake
UDASA yageuka mbogo, yauvaa uongozi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam