October 25, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Chadema yataka Heche achiwe huru

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema Makamu Mwenyekiti wake wa taifa, John Heche, anashikiliwa kwenye mahabusu ya Polisi, iliyopo Mtumba, mkoani Dodoma. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dares Salaam … (endelea).

Katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika, ameliambia MwanaHALISI Online, kwamba kiongozi huyo, anashikiliwa na polisi kwa madai ya kukiuka sheria za uhamiaji.

Amesema, “…mheshimiwa Heche amehojiwa na Idara ya uhamiaji mbele ya wakili wa chama na kaka yake akituhumiwa kuvunja sheria za uhamiaji kwa kile walichokisema alivuka mpaka wa Tanzania na kuingia nchini Kenya bila kufuata taratibu.”

Kwa mujibu wa Mnyika, pamoja na kosa hilo kutajwa kuwa na dhamana, jeshi la polisi limekataa kumpa dhamana Heche, kwa kusema, “kuna maelekezo kutoka juu.”

Kwamba, mwanasiasa huyo wa upinzani anayekaimu nafasi ya mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini, aendelee kubaki mahabusu. ilieleza taarifa hiyo.

Heche alikamatwa na polisi siku ya Jumatano kwenye lango la kuingilia Mahakama Kuu, jijini Dar es Salaam kabla ya kupelekwa kituo kikuu cha Polisi Kati, Dar es Salaam kisha kusema wanampeleka mkoani Mara.

MwanaHALISI Online limeshindwa kumpata msemaji wa jeshi la polisi, kuzungumzia madai hayo ya Chadema.

Hata hivyo, tangu kuanza kwa mwaka huu, mamia ya viongozi wa Chadema wamekamatwa na polisi na kufunguliwa mashitaka mbalimbali, wengine kuchukuliwa na wanaoitwa na serikali, “watu wasiofahamika,” huku baadhi yao wakiwa hawajulikani waliko mpaka sasa.

Chadema kimekuwa kikilalamikia vitendo hivyo na kusema, “ni muendelezo wa mpango wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), chini ya Rais Samia Suluhu kuwakamata viongozi wake na kuwaweka kizuizini,” ili kupunguza nguvu ya chama chao.

Kufuatia hali hiyo, Mnyika anasema, “tunamtaka Rais Samia kuacha kutumia vyombo vya dola kukamata na kuwaweka kizuizini washindani wake wa kisiasa.”

Kukamatwa kwa Heche, kunakifanya Chadema kuwa na viongozi wake wawili wajuu kuzuiliwa. Mwingine anayeshikiliwa ni Tundu Lissu, anayetuhumiwa kupanga uhaini.

About The Author

error: Content is protected !!