October 25, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Wassira: Si haki kuzuia watu kwenda kupigakura

 

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema moja ya sharti la haki za binadamu ni kutowazuia wengine kupata haki yao ya kikatiba ikiwemo kupiga kura kuchagua viongozi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kagera … (endelea).

Amesema CCM inaheshimu haki za binadamu, lakini atakayeshindwa kuziheshimu na kusababisha uvunjifu wa sheria, atashughulikiwa kwa kadri sheria inavyoelekeza.

Kiingozi huyo amewahakikishia Watanzania kwamba kila mwenye sifa atapata fursa ya kupiga kura kwa amani na utulivu na kwamba hakuna yeyote atakayezuia uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu kumchagua rais, wabunge na madiwani.

Wassira ametea kauli hiyo leo, tarehe 24 Oktoba 2025 alipokuwa akizungumza na wana CCM kutoka Wilaya ya Bukoba, mkoani Kagera akiwa katika ziara ya kumnadi mgombea urais Samia Suluhu Hassan, ubunge na udiwani.

“Wenye matatizo madogo madogo sisi tunawaambia wanazungumza sana haki za binadamu na sisi tunawaambia tunaziheshimu, lakini haki za binadamu zina masharti na masharti yake ni kwamba kama unadai haki yako wewe usiwazuie wengine kupata haki zao,” amesema.

Wassira amesema kuwa, mgombea urais wa CCM ameahidi ndani ya siku 100 baada ya uchaguzi, ataanza kukaa pamoja na wanaohitaji kuzungumza naye juu ya mambo wanayoona hayako sawa.

“Sisi hatujakataa kusikiliza hata kidogo, mgombea wetu amesema katika siku zake 100 baada ya uchaguzi ataanza mjadala na wale ambao wanahitaji kuzungumza naye, maana hatuendeshi nchi kwa mabavu tunaendesha kwa mazungumzo.

“Kwa hiyo kama kuna mmoja anafikiri yeye ana mawazo lakini hayajasikilizwa bado nafasi ya kusikilizwa ipo, huwezi kusema utafanya fujo kwa sababu hujasikilizwa, utashughulikiwa kwa sababu kuna kusikilizwa lakini kama hutaki kusikilizwa unashughulikiwa ili walio wengi wapate amani maana ni haki yao kupiga kura.

“Sheria zipo zinasema watu wakienda kupiga kura hakuna anayeruhusiwa kuwashawishi kimyakimya au hata waziwazi kwamba wasiende kupiga kura, anaingilia haki yao,” alieleza.

Kwa mujibu wa Wassira, kupiga kura ni haki ya kila mwananchi mwenye sifa lakini haipaswi kutumika vibaya kwa baadhi ya watu kuwahadaa na kuwashurutisha wengine kutotimiza haki hiyo.

“Anayeleta maneno mwambieni sheria zipo kwa hiyo una haki ya kukataa kwenda kupiga kura ni haki yako, lakini usiwaambie wengine wasiende, ukiwaambia unavunja haki zao, nilitaka tuelewane kwa hilo kwa sababu vinginevyo tutakuwa tunahangaishana,” amesisitiza.

Amesema wapo baadhi ya watu wasioitakia mema CCM na nchi kwa ujumla wanahoji kwa nini chama kimemteua Rais Samia kuwania nafasi hiyo na kwamba jibu lao ni kuwa, hilo limefanyika kutokana na sifa na uwezo alionao kuongoza Watanzania.

Wassira amesema kuwa; “Wako wengine ambao hawatutakii mema wanasema kwa nini tulimteua Samia kugombea na sisi tunawaambia mbona Samia anakubalika kwa wananchi na sifa moja ya kuteua ni kukubalika, Mwalimu Julius Nyerere alituasa alisema chama ambacho hakisikilizi watu kitalia machozi halafu kitakosa mtu wa kukifuta.”

“Sisi tumemchagua Samia kwa sababu anakubalika na wananchi na ushahidi ni kupokelewa kila anakopita, hivi watu hao mlikuwa mnawaswaga na polisi kwenda kumpokea, siwalikuwa wanakuja wenyewe?.

“Kwa hiyo anayo sifa ya kukubalika, anayo sifa kubwa ya kusimamia utekelezaji wa maendeleo ya watu, hizo ndizo sababu zetu na sababu hizo ni za msingi. Kwa hiyo kama wewe humkubali sisi hatuna matatizo na wewe, ukae tu maana hata kupiga kura ni hiyari kama una matatizo sana unaweza ukalala siku hiyo maana utapata nafuu zaidi kuliko kuhangaika lakini watakaokwenda watakuchagulia rais, watakuchagulia diwani watakuchagulia na mbunge sasa usije ukaamka mbunge gani huyu, wewe hukwenda wenzako wamechagua,” amesema.

About The Author

error: Content is protected !!