
MWILI wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Amollo Odinga, umewasili mjini Kisumu, magharibi mwa Kenya na tayari umefikishwa katika uwanja wa michezo wa Jommo Kenyatta. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kisumu, Kenya … (endelea).
Raila alianza safari yake ya mwisho duniani kutokea uwanja wa kimataifa wa Jommo Kenyatta jijini Nairobi, ambapo mwili wake, ulibebwa na ndege ya kijeshi aina ya SPARTAN kutoka kambi ya jeshi la nchi kavu lnalopakana na uwanja wa JKIA.
Shughuli nzima inaongozwa na jeshi la Kenya (KDF), ambapo maafisa wakuu wa jeshi wamesimamia usafiri wa mwili huo ambao uliwasili katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Kisumu, majira ya saa moja na nusu asubuhi.
Ulipokelewa na Meja Jeneali Jospeh Nyaga, Afisa msimamizi wa kambi za jeshi la nchi kavu katika ukanda wa magharibi mwa Kenya.
Luteni Kanali Baraza ambaye ni msimamizi wa maafisa wa jeshi wanaoulinda na kuubeba mwili wa Odinga, alishuka kwenye ndege kwanza na kukikongoza kikosi chacke cha mafisa wenye hadhi ya meja kuandaa jeneza hilo kwa usaidizi wa maafisa wengine wa kijeshi.
Shughuli ya kuondoa mwili kutoka kwenye ndege hilyo ya usafiri wa mizigo na wanajeshi kwa shughuli zao za kawaida nchini Kenya na vitani, ilikuwa na utaratibu uliofuatwa kwa ufasaha huku wanajeshi wakihakikisha kwamba yote yanakwenda vyema.
Baada ya karibu nusu saa, jeneza lilisukumwa kwa kigari chenye magurudumu mawili makubwa cha kubebea maiti na kupelekwa kwenye ndege nyingine ya kijeshi aina ya helikopta ya Bell UH -1.
Ndege hiyo, iliupokea mwili na kuubebba hadi uwanja wa michezo wa Jommo Kenyatta Mamboleo ambako kumejaa waombolezaji walioanza kuwasili eneo hilo, kuanzia saa kumi za alfajiri.
Ndege hiyo ilipaa angani kwa muda mfupi tu, kama dakika 8 hivi, huku watu wengi wakishangaa kwa nini hatua hiyo imechukuliwa na serikali.
Hata hivyo, huenda idadi kubwa ya watu iliyopo kwenye barabara kuu ya kutoka uwanja wa ndege wa Kisumu ni mkubwa na vitengo vya usalama visingetaka yaliyoshuhudiwa Alhamisi katika uwanja wa ndege wa Jommo Kenyatta, jijini Nairobi, yatokee tena Kisumu.
Wananchi walisimama kando kando ya barabara nje ya uwanja wa Kisumu wakiwa na matumaini ya kuuona mwili ukipita barabarani, lakini hawakuweza kufanikiwa.
Lakini taarifa watu wengi wanatarajiwa kupata fursa ya kumuaga Raila mara baada ya shughuli hiyo itakapoanza rasmi katika uwanja huo.
Wakenya watautazama mwili kati ya saa tatu asubuhi na saa kumi na mbili jioni, ambapo Raila Odinga ataanza safari ngumu kabisa ya kuelekea alikozaliwa kule Bondo usiku wa leo na kulazwa katika boma lake la Opoda Farm alikoishi na familia yake.
Odinga atazikwa kando ya baba yake Jaramogi Oginga Odinga – aliyekuwa Makamu wa Rais wa kwanza wa Kenya – aliyefariki dunia mwaka 1994.
Familia imesema baada ya ibada ya mazishi itakayoandaliwa Jumapili, ni watu wachache tu watakaoingia katika eneo la makaburini na kushuhudia mwili wake ukishuhswa chini na kuzikwa.
Wananchi watashuhudia shughuli hiyo kwenye runinga kubwa kubwa ambazo zitawekwa katika shule za msingi na upili ambazo ziko karibu na makazi ya Kango’ KA Jaramogi ambako ni boma la mzee Jaramogi na makao ya familia kubwa ya Odinga.
Raila ambaye alikuwa mwanasiasa mashuhuri nchini Kenya aliye na takriba miaka 35, alihudumu kama Waziri Mkuu na kuweka rekodi ya pekee ya kusimamia demokrasia na utawala wa sheria nchini mwake.
Amewahi kuwania urais kwa zaidi ya mara tano, lakini hakuwahi kufanikiwa kushinda.
Atakumbukwa kwa mchango wake wa mabadiliko ya kikatiba, uanaharakati wake wa kutetea haki za wa Kenya na juhudi zake za upatanishi ndani na nje ya nchi.
ZINAZOFANANA
Mambo matano makubwa kuhusu Raila
Raila Odinga alikuwa mwanaharakati wa demokrasia – Barack Obama
TMA yatangaza utabiri wa mvua za msimu