September 10, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Rais Samia azidi kumwaga ahadi Igunga

Dk. Samia Suluhu Hassan

 

MGOMBEA urais, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi wa Igunga kuunga mkono chama chake, kuekea uchaguzi mkuu ujao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Tabora … (endelea).

Akizungumza mjini Igunga leo, tarehe 10 Septemba 2025, Samia alidai kuwa utekelezaji wa Ilani ya CCM (2020 – 2025), umeleta mafanikio makubwa.

Akaahidi maendeleo mengine makubwa zaidi yatapatikana, ikiwa kuboresha maisha ya kila mwananchi, kupitia Ilani ya uchaguzi ya mwaka huu.

Kwa mujibu wa Samia, wilaya ya Igunga, imepata mafanikio makubwa katika sekta ya afya, ikiwemo ukarabati wa hospitali ya Halmashauri na kukamilika kwa ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi.

Amesema, kukamilika kwa jengo hilo, kumesaidia kuboresha huduma za afya kwa wagonjwa.

Katika sekta ya elimu, idadi ya shule za msingi na sekondari imeongezeka, huku Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Stadi (VETA), kikiwa ni jukwaa muhimu la kuwajengea vijana ujuzi wa kiufundi na stadi za maisha.

Sekta ya kilimo na biashara imeimarishwa kwa ongezeko la uzalishaji wa mazao ya chakula, upatikanaji wa mbolea na kuendelezwa kwa viumbeaji na uzalishaji wa vifaranga vya samaki.

Aidha, mtandao wa barabara mjini na vijijini umeboreshwa, ili kurahisisha usafirishaji wa wananchi na bidhaa zao, jambo linaloongeza mapato na fursa za biashara.

Baada ya kufafanua mafanikio, Dk. Samia alitoa ahadi zinazolenga kusukuma mbele maendeleo. Ahadi hizo ni pamoja na ujenzi wa vituo viwili vya afya Uswaya na Kining’inila.

Mengine aliyoahidi, ni ukamilishaji wa maboma ya madarasa 180 katika shule za msingi, maboma ya maabara 20 katika shule za sekondari na nyumba 37 za walimu.

Vilevile, Rais Samia ameahidi ujenzi wa mabwawa na skimu katika vijiji vya Igurubi, Buhekela, Simbo, Itumba, Mwamapuli, Mwalunili, Makomelo na Mwashiku.

Ameahidi ujenzi wa Soko Kuu la wafanyabiashara wadogo na wakubwa, maboresho kwenye maeneo ya uwekezaji na kukamilisha maboma ya majosho 15 pamoja na mabirika ya kunyweshea mifugo.

Katika sekta ya michezo, ujenzi wa kiwanja cha michezo cha halmashauri ya Igunga na jengo jipya la ofisi za Halmashauri unaendelea, kuimarisha burudani, michezo na utendaji bora wa utawala

About The Author

error: Content is protected !!