September 8, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mkituchagua tena tutaendelea kutoa ruzuku ya mbolea

 

MGOMBEA Urais na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesema ikiwa watanzania watampa ridhaa ya kuongoza tena kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, serikali yake itajikita katika kuendelea kukuza uzalishaji na tija kwa wakulima nchini kwa kuendelea kutoa ruzuku za mbolea na pembejeo pamoja na ujenzi wa miundombinu saidizi kwa wakulima. Anaripoti Mwandishi Wetu, Iringa … (endelea).

Rais Samia amebainisha hayo leo Jumapili tarehe 7 Septemba 2025, akiwa Iringa Mjini kwenye uwanja wa Samora, akisema kuwa mara ya mwisho kufika Mkoani humo ilikuwa Agosti 2022 ambapo pamoja na mambo mengine amefanikisha utekelezaji wa ahadi zake za ujenzi wa skimu za umwagiliaji kwa wakulima.

“Mkitupa ridhaa tutaendelea kutoa ruzuku ya mbolea na pembejeo kote nchini, tutajenga vituo 50 vya kuhifadhia mazao ya parachichi, tutajenga vituo vingine vya baridi vya kuhifadhia mazao ya mbogamboga, tutajenga maghala ya kuhifadhia mazao ya chakula na biashara, tutaanzisha vituo vya ukodishaji zana za kilimo ili wakulima waweze kupata huduma za kilimo kwa bei nafuu kwani vituo vyetu vitakuwa nusu bei ya inayotozwa na sekta binafsi,” amesema Samia

Rais Samia amesema jitihada zilizofanywa na serikali yake kwa awamu ya kwanza zimewezesha uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kuongezeka ikiwemo uzalishaji wa zao la Kahawa Mkoani Iringa ambapo uzalishaji umeongezeka kutoka Tani 109 mwaka 2020 hadi kufikia Tani 323 mwaka 2025, kando ya ongezeko kubwa la zao la Mpunga linaloshuhudiwa kwenye Mikoa ya Kusini Magharibi mwa Tanzania.

Aidha jitihada hizo pia zimeiwezesha Tanzania kuwa mzalishaji wa pili wa zao la Mahindi Barani Afrika, ikizalisha tani Milioni kumi, akisisitiza kuwa dhamira yake ni kuendelea kukuza uzalishaji na tija kwa wakulima kupitia ruzuku za mbolea na pembejeo pamoja na miundombinu mingine wezeshi.

About The Author

error: Content is protected !!