July 12, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Vita vya Gaza: Hamas waapa kufia kwenye ardhi yao

 

KUNDI la wanamgambo wa Hamas, wametangaza kutounga mkono makubaliano yoyote ya usitishaji mapigano yatakayoruhusu jeshi la Israel kuendelea kuwepo Ukanda wa Gaza. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Taarifa kutoka mjini Doha, kunakofanyika mazungumzo ya kusitisha mapigano kwa muda wa siku 60, huku Israel na Hamas, wakiendelea kujadiliana kuhusu uwezekano wa kusita vita.

Hamas imetoa pendekezo la kuwaachia mateka kumi (10) waliokamatwa tarehe 7 Oktoba 2023, lakini wanalalamikiwa vikwazo vya misaada na kutokuweko hakikisho la usitishaji kamili wa vita Ukanda wa Gaza.

Bassem Naim, afisa mwandamizi wa Hamas, amesema kundi hilo haliwezi kukubali ardhi ya Palestina kuendelea kutawaliwa chini ya udhibiti wa Israel.

Msimamo huo ndio unaowasilishwa kwenye mazungumzo ya Doha, likiwa linapinga hasa udhibiti wa Israel, katika mji wa Rafah na njia ya Morag.

Aidha, Naim amesema Hamas inataka kusitishwa kwa mfumo wa sasa wa usambazaji misaada unaoungwa mkono na Marekani na Israel, kwani unahatarisha maisha ya Wapalestina na kusababisha vifo vya raia wanaotafuta misaada.

Katika tukio la kusikitisha, mashambulizi ya Israel yamewaua watu 17, wakiwemo watoto wanane na wanawake wawili, katika eneo la Deir el-Balah katikati mwa Gaza.

Jeshi la Israel lilidai kuwa lilikuwa likimlenga mwanamgambo wa Hamas aliyeshiriki uvamizi wa 7 Oktoba 2023. Limeahidi kufanyia uchunguzi tukio hilo na kusisitiza kuwa linafanya kila juhudi kupunguza madhara kwa raia.

Daktari wa Hospitali ya Mashahidi ya Al-Aqsa na msemaji wa Wizara ya afya Gaza, Khalil al-Deqran amesema, shambulio la Israel kwenye kituo cha afya limesababisha vifo kadhaa miongoni mwao ni watoto sita na kujeruhi wengine kadhaa.

“Jeshi la uvamizi limefanya mauaji makubwa leo asubuhi katika kambi ya Deir al-Balah, ambapo lilishambulia raia katikati mwa eneo hilo,” ameeleza na kuongeza, “…mashahidi 15 waliwasili Hospitali ya Al-Aqsa, wakiwemo watoto sita.”

Alisema, hospitali hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa na mafuta, na huenda ikasitisha huduma muda mfupi ujao kwa sababu ya jeshi la uvamizi kuzuia mafuta kuingia kwa kiwango cha kutosha.

Yousef Al-Aydi, mmoja wa mashuhuda wa shambulizi hilo, ameeleza kuwa wakati wa tukio, watu wengi walikuwa wamekusanyika mbele ya kituo cha afya kusubiri virutubisho vya lishe.

“Ghafla tulisikia sauti ya droni ikikaribia, kisha mlipuko mkubwa ukatokea. Ardhi ilitetemeka, na kila kitu kiligeuka kuwa damu na vilio vya kuogofya,” ameeleza kwa sauti ya masikitiko.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya (EU), Kaja Kallas, amesema kuwa Israel imekubali kuchukua hatua madhubuti za kuboresha hali ya kibinadamu huko Gaza.

Hatua hizo ni pamoja na kuongeza idadi ya malori ya misaada, kufungua vituo zaidi vya mpakani, kuruhusu tena mafuta kwa ajili ya vituo vya kibinadamu, na ulinzi wa wahudumu wa misaada.

Amesisitiza kuwa misaada hiyo lazima ifikishwe moja kwa moja kwa raia na kwamba hatua zitachukuliwa kuhakikisha hakuna misaada inayoishia mikononi mwa Hamas.

Hadi sasa, serikali ya Israel haijathibitisha rasmi utekelezaji wa hatua hizo, lakini umoja huo wa ulaya unasema, unatarajia serikali ya Benjamin Netanyahu, itatekeleza kila ahadi waliyoitoa.

Bali pamoja na kuwapo matumaini ya kufungwa makubaliano ya muda, vita vya Gaza vinaendelea kuleta maafa makubwa kwa raia, huku juhudi za upatanishi zikiendelea bila mafanikio hadi sasa.

About The Author

error: Content is protected !!