June 22, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Prof. Kitila awataka waandishi kusimamia misingi katika uchaguzi

Profesa Kitila Mkumbo

 

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amewataka waandishi wa habari kusimamia misingi ya uandishi wa habari katika kipindi hiki cha uchaguzi, ili kuhakikisha nchi inabakia na amani na umoja. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Prof Kitila amesema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DPC), uliofanyika kwenye katika Ukumbi wa Karimjee.

Amesema waandishi wa habari wana wajibu wa wakutenda haki kwa wadau wote katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Waziri Kitila amesema haki ya kwanza inapaswa kuanzia kwenye kuitazama Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kwa kuzingatia majukumu ya Kikaiba na Kisheria.

Pia amewataka watendee haki vyama vya siasa vyote wakati wa kampeni na hata baada ya hapo.

“Nawaomba mtoe taarifa sahihi iwe, inaumiza au kufurahisha mhusika. Kimsingi mnatakiwa mtoe taarifa za kitafiti ambazo zinaenda kuleta mabadiliko kwa jamii,” amesema.

Waziri Kitila amesema pia waandishi wa habari wana jukumu la kudumisha amani, kwani amani ikiyumba kuirudisha ni kazi ngumu.

“Ni lazima mzingatie maslahi ya Taifa kwenye uandishi wenu,” amesema.

Amesema pia waandishi wa habari wanapaswa kuandika habari za uwajibikaji kwa viongozi na serikali, ili kuhakikisha ahadi zote zinatekelezwa.

“Wananchi wanahitaji watetezi na watetezi wao ni waandishi wa habari na wanasiasa wanaowawakilisha,” amesema.

Pia amesema waandishi wa habari wana wajibu wa kukuza ushirikishwaji kwenye utekelezaji wa majukumu yaliyopangwa ikiwemo kuleta maendeleo.

Amesema waandishi wa habari wanapaswa kuwa vioo kwenye demokrasia, ikiwemo kuchaguana ili wawe na uhalali wa kuhoji wengine ambao wanawaandika.

“Lazima tujenge utamaduni wa kidemokrasia ambao unahitaji, uwazi, kukosoana, kujifunza, kuwajibika na mengine mengi,” amesema.

Waziri Kitila amesema uaandishi wa habari una umuhimu duniani kote kwa kuumba mtazamo na mwelekeo wa jamii.

Alisema iwapo waandishi wa habari wakiharibu jamii itaharibika.

“Waandishi wa habari, wanasiasa na viongozi wa dini ni makundi ambayo lazima yasikike na hayaepukiki kwenye jamii, upende usipende,” amesema.

Prof Kitila amesema makundi hayo matatu ndio yanatengeneza mtazamo wa jamii kwenye kila kitu, ikiwemo maendeleo, kwani watu hao wakisema tofauti ni wazi kuwa hali inakuwa kinyume.

Amesema uandishi wa habari, mwanasiasa na viongozi wa dini ni lazima wajiheshimu na kuwa na utu ili wawe mfano kwa jamii.

Waziri amesema waandishi wa habari wanawajibu wa kuhamasisha mifumo ya kidemokrasia jambo ambalo Tanzania linafanyika.

Amesema uhuru na amani iliyopo nchini kwa asilimia kubwa imechangiwa na waandishi wa habari kwa kufuata sheria na kanuni kwenye kazi zao.

Aidha, amesema uchaguzi ni kilele cha kuonesha demokrasia na kwamba moja ya muamuzi wa uchaguzi ni waandishi wa habari na hiyo itaunga mkono dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuona uchaguzi huru, amani na wenye kuacha umoja kwa Watanzania.

Waziri Kitila amesema Rais Samia anaamini katika vyombo vya habari na ndio maana Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 wametambua sekta hiyo.

Alisema hata ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametambua vyombo vya habari kama nyenzo muhimu ya kuwajibisha serikali.

Amewataka wana DPC kulinda chama chao, ili kudumisha umoja na mshikamano baina yao.

“Nawaomba waandishi wa habari mjenge utamaduni wa kutafuta na kusambaza maarifa, ili jamii iweze kufaidika na taaluma yenu,” amesema

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DPC), Bakari Kimwanga akimkaribisha Waziri Kitila alimhakikishia kuwa waandishi wa habari watafanya kazi kwa weledi kipindi cha uchaguzi.

Aidha, Kimwanga ameiomba Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), iongeze siku 10 kwa ajili ya usajili wa waandishi.

Amesema waandishi wamepewa muda mfupi wa mwezi mmoja kujisajili JAB, ili hadi sasa mwitikio sio mzuri kutokana na changamoto za kiufundi, hivyo anaomba muda uongezwe.

Mwenyekiti huyo amemuomba Waziri Kitila kuwasiliana na Waziri mwenzake wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi ili kuhakikisha muda unaongezwa hata kwa siku 10.

Pia kiongozi huyo wa DPC amemuomba Waziri Kitila kuhakikisha ahadi ya serikali kulipa madeni ya vyombo vya habari ili vyombo hivyo kuwa na uchumi imara.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, SACP John Malulu amesema jeshi la polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam litatoa ushirikiano mkubwa kwa waandishi wa habari na kwamba milango ipo wazi.

SACP Malulu amesema vyombo vya habari ni muhimu katika kuweka usalama katika nchi hivyo watashirikiana nao kwa nguvu zote.

About The Author

error: Content is protected !!