
Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Akama Shaaban
AFISA Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Akama Shaaban amewataka Maofisa (10) na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi mmoja, kwenda kuvitendea haki vyeo vyao walivyovipata kwa Jamii kwa kuyaishi na kutekeleza mambo yenye tija ikiwa ni pamoja na kutekeleza majukumu hayo wakiwa na hofu ya Mungu ili kutoa haki na kuyafanya kwa vitendo yale yote waliyofundishwa wakiwa mafunzoni. Anaripoti Issa Mwadangala, Songwe … (endelea).
Rai hiyo imetolewa tarehe 16 Juni 2025 katika ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, wakati akiongea na Maofisa na Mkaguzi ambao waliomaliza mafunzo yao ya uongozi tarehe 9 Juni 2025, katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam (DPA) ambayo mafunzo hayo yalifungwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Mnapotekeleza majukumu yenu katika kazi za kila siku fanyeni huku mkiwa na hofu ya Mungu bila kusahau kufanya kazi kwa nidhamu kwa kuwatendea haki wateja wa ndani na nje ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na miongozo na kuwa waadilifu bila kuwa na muhali na mtu yoyote ili jamii iendelee kuwa salama,” alisema ACP Akama.
Kwa upande wake, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Johny Maro amewataka Maofisa hao kwenda kusimamia nidhamu kwa askari waliochini yao pamoja na ufuatiliaji wa majalada ya kesi na kuyakamilisha kwa wakati kwa kufuata utaratibu ili jamii iendelee kuliamini Jeshi la Polisi na kuweza kupata taarifa fiche za uhalifu na wahalifu kwa lengo la Mkoa wa Songwe kuendelea kuwa salama.
Naye, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Joseph Bukombe aliwataka maofisa hao kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya uhalifu na ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kutoa huduma bora kwa wateja ili kuendelea kujenga taswira nzuri ya Jeshi la Polisi.
ZINAZOFANANA
IGP Wambura afanya mabadiliko ya maofisa ndani ya jeshi la Polisi
Mahakama yakubali ombi la serikali kukatisha ushahidi wa kwanza kesi ya Lissu
‘Polisi wanaiba kura’ ilivyomuibua shahidi wa serikali