
WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe ametoa wito kwa wasafirishaji wote wa Kitanzania wanaosafirisha bidhaa za kilimo, kuacha kupakia bidhaa hizo mpaka hapo Malawi na Afrika Kusini watakapo badilisha msimamo wao. Anaripoti Apaikunda Mosha, Dar es Salaam … (endelea).
Ameandika hayo katika ukurasa wake wa X hii leo tarehe 17 Aprili 2025, Bashe amewataka na kuwashauri wafanyabiashara walioweka order za apples, machungwa, na bidhaa zingine ambazo hununuliwa Afrika kusini, kuacha kwa sasa kwani hatutoziruhusu kuingia Tanzania mpaka hapo Afrika Kusini itakapo tufungulia soko la ndizi.
Amesema hii imetokana na taarifa rasmi ambayo serikali imepokea kuwa serikali ya Malawi imezuia kuingia kwa mazao ya kilimo kutoka Tanzania, yakiwemo unga, mchele, tangawizi, ndizi, na mahindi. Hatua ambayo imeathiri moja kwa moja shughuli za wafanyabiashara wetu wanaosafirisha bidhaa hizo kwenda Malawi.
“Ni vyema ifahamike kuwa kwa kipindi cha miaka mitano, Serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kufungua soko la ndizi nchini Afrika Kusini bila mafanikio. Hali hii inafanana na changamoto tulizopitia kwa zaidi ya miaka kumi katika kufungua soko la parachichi, hadi pale tulipoamua kuchukua hatua za kulinda maslahi ya nchi yetu,” amesema Bashe.
Aidha waziri Bashe ameeleza kuwa kutokana na hali hiyo, na baada ya juhudi zote za kidiplomasia kufanyika bila mafanikio, serikali ya Tanzania imeamua kuweka misimamo yake kwa nchi hizo.
Ameeleza, ”Iwapo Serikali ya Malawi na Afrika Kusini hazitabadilisha msimamo wao kufikia Jumatano ijayo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo itazuia uingizwaji wa mazao na bidhaa zote za kilimo kutoka nchi hizo mbili.”
Vilevile mizigo ya bidhaa za kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini haitaruhusiwa kupita ndani ya mipaka ya Tanzania, kuelekea bandari ya Dar es Salaam au nchi nyingine yoyote, hadi zuio hilo litakapoondolewa, na hata usafirishaji wa mbolea kwenda Malawi utasitishwa, ikiwa ni sehemu ya hatua za kulinda maslahi ya wakulima na wafanyabiashara wa Kitanzania.
“Ninathibitisha kuwa kama Waziri mwenye dhamana, nimewasiliana kwa njia mbalimbali na Waziri wa Kilimo wa Malawi bila mafanikio ya kupata majibu rasmi. Hatua hizi ni za kulinda heshima ya nchi yetu, uchumi wa wakulima wetu, na usawa katika biashara za kikanda,” amesema Bashe.
ZINAZOFANANA
Mbezi juu yashikwa mkono na Meridianbet
Chadema: Tundu Lissu yupo gerezani Ukonga
Serikali yajivunia mafanikio sita ya TASAF