
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefungua rasmi shule ya sekondari ya wasichana katika wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, ameomba shule hiyo iitwe kwa jina la Hayati Waziri Betrice Shelukindo kwa sababu alikuwa akipambania haki za wasichana wengi. Anaripoti Apaikunda Mosha, Kilindi-Tanga … (endelea).
Baada ya uzinduzi huo mapema leo 25 Februari 2025 Rais alipata wasaa wa kutoa hotuba fupi kwa wakazi wa Tanga na ameeleza dhamira ya serikali ya katika kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia hapa nchini.
Amesema shule hiyo ina jumla ya mabweni 12 ambayo baadhi ya hayo yamekamilika huku mengine yakiwa hatua za mwishoni kukamilika, jambo ambalo litasaidia kupunguza changamoto kwa wanafunzi hao ya kutembea umbali mrefu wakati wa kwenda shule.
Vilevile Rais Samia ameeleza namna alivyofurahishwa na uwepo wa Darasa la TEHAMA shuleni hapo, jambo ambalo litawasaidia wanafunzi wengi kujua na kujifunza teknolojia mapema ili waweze kushindana katika soko la ajira la kisasa.
Aidha, Rais Samia amezungumzia miradi mingine ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika wilaya ya Kilindi, amesema upo ujenzi wa hospitali ya wilaya, vituo vya afya, soko la madini, mashamba ya malisho ya mifugo, na ujenzi wa barabara ya Handeni-Kiberashi-Kijungu-Chemba-Kwa Mtoro-Singida yenye urefu wa kilomita 461.
Mwisho kabisa Rais Samia amemtaka Waziri wa Ardhi kuweka kambi Kilindi ili kushughulikia migogoro ya ardhi, ambayo mingine inasababishwa na viongozi, pamoja na matatizo yaliyosababishwa na GN ili wakazi wa Kilindi waendelee kuishi bila migogoro ya ardhi.
ZINAZOFANANA
Kampasi ya Mzumbe kujengwa Mkinga, mkoani Tanga
Vodacom Foundation kufadhili kongamano la Utafiti wa Elimu Tanzania 2025
Sekretarieti ya Ajira yatoa ufafanuzi ajira za walimu