![](https://mwanahalisionline.com/wp-content/uploads/2025/02/WhatsApp-Image-2025-02-10-at-18.33.24.jpeg)
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dk. Hassan Abbas
WADAU wa Malikale nchini wametakiwa kujadili marekebisho ya kanuni za Malikale na Makumbusho bila kusahau namna zitakavyowezesha matumizi ya teknolojia ya kisasa ya Mawasiliano katika uhifadhi na kutangaza vivutio vya Malikale na Makumbusho ili kuendana na wakati uliopo hali itakayosaidia uhifadhi endelevu na kuvutia watalii wengi zaidi katika maeneo hayo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dk. Hassan Abbas katika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, Jijini Dar es salaam alipokuwa akifungua kikao kazi kati ya wataalam wa Wizara hiyo na wadau wa Malikale nchini kujadili Kanuni za Utekelezaji wa Sheria ya Mambo ya Kale Sura ya 333 kwa lengo la kufanyia maboresho.
Dk. Abbasi amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan anaendelea kufanya kazi kubwa katika sekta ya Maliasili na Utalii hali inayochochea ongezeko la watalii katika vivutio vilivyopo nchini, hivyo ni vyema kwa wadau wa Malikale kuunga mkono juhudi hizo kwa kuvitangaza vivutio hivyo kisasa zaidi ili kuondoa mitazamo ya baadhi ya watu kuwa Malikale ni vitu vilivyopitwa na wakati.
“Kwa sasa tunayaona ni Magofu lakini tunafanyaje ili vijana wa sasa wayaone kuwa Jokofu?, maana sote tunajua vijana wanakimbilia kwenye Jokofu kwa kuwa kuna vitu vizuri vya kuvutia hivyo sasa kwa nini magofu yabakie tu vitu vya kale tu katika ulimwengu huu wa usasa? Sasa angalieni kanuni hizi zinawezeshaje vivutio vya malikele kibiashara zaidi?” Alisisitiza Dk. Abbas.
Dk. Abbas ameongeza kuwa ni matumaini ya Uongozi wa Wizara ya Maliasili Utalii kuwa maoni hayo yatasaidia kuboresha kanuni zinazopendekezwa ili ziweze kuakisi mahitaji halisi ya uhifadhi wa malikale kijamii na kiuchumi.
Aidha Dk. Abbas alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha wadau wa Malikale, kuchangamkia furusa iliyopo kwenye Tuzo za Utalii zilizozinduliwa hivi karibuni, kwa kushiriki vyema kwenye uhifadhi wa malikale na Makumbusho, kutangaza sekta hiyo ili kuvutia watalii wengi zaidi na kisha kuingia kwenye kinyang’anyiro cha Tuzo hizo za kipekee nchini.
Akizunguza juu ya kikao kazi hicho Mkurugenzi wa Idara ya Malikale nchini, Dk. Kristowaja Ntandu amesema, kama Idara inayosimamia sheria na kanuni mbalimbali za Malikale, wameona ni vyema mabalidiko hayo yatokane na ushiriki wa wadau ili kuwezesha utekelezaji wa pamoja kati ya Wizara na wadau hao.
Katika hatua nyingine, Dk. Ntandu ametoa wito kwa wadau hao kuhakikisha wanatumia fursa hiyo adhimu ili kutoa maoni yatakayozingatia uhifadhi endelevu kwa maslahi mapana ya Taifa na Jamii kwa ujulma.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dk. Noel Lwoga amepongeza jitihada za Wizara katika kuhakikisha sekta ya Malikale na Makumbusho inakuwa zaidi hususani katika maboresho ya kanuni hizo ambazo kimsingi zinakwenda kuhamasisha jamii kuanzisha makumbusho binafsi hali itakayotanua wigo wa uhifadhi na urithi wa malikale na historia.
Sheria ya Mambo ya Kale, Sura 333 ilitungwa mwaka 1964 na kufanyiwa marekebisho kwa mara ya kwanza mwaka 1979 na baadae kufanyiwa maboresho mwaka 2022. Miongoni mwa marekebisho yaliyofanyika mwaka 2022 ni kuimarisha mifumo ya kitaasisi kwa ajili ya kusimamia sekta ya malikale
ZINAZOFANANA
Usalama mtandaoni ni amani kwa Taifa
Dk. Mpango mgeni rasmi kikao kazi cha Serikali mtandao
Waziri Chana afungua rasmi onyesha la wiki ya Ubunifu wa Italia