WAKATI Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika TLS, ukitarajiwa kufanyika kesho Ijumaa na kumpata Rais wa kukiongoza chama hicho miaka mitatu, wakili Julius Mtatiro na Ally Kileo wamewachambua kwa undani wagombea hao sita. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Mawakili hao wanaogombea kwenye uchaguzi huo ni pamoja na Boniface Mwabukusi, Ibrahim Bendera, Emmanuel Muga, Revocatus Kuuli, Paul Revocatus Kaunda, na Sweetbert Nkuba.
Mtatiro kwenye taarifa yake leo amesema wagombea wote 6 waliofuzu ni wazoefu na wana sifa mbalimbali za kiuongozi kwani kila mmoja ana sifa za kipekee tofauti na wenzake na kila mmoja akiwa na uzoefu wa kipekee ambao si lazima ufanane na mwingine, na kwa hiyo ni wazi kuwa kila mgombea anaweza kuleta mabadiliko fulani au matatizo fulani atakavyopata nafasi ya kuhudumu urais wa TLS.
Alisema kabla hawajafanya uchambuzi huo walikuwa na maswali mbalimbali vichwani mwao ambayo watayatumia kama msingi wa kile kinachoweza kutokea TLS na mwelekeo wake kwa siku zijazo na kwamba miongoni mwa maswali hayo ni Je, TLS inahitaji Rais wa namna gani kwa muktadha wa sasa wa nchi yetu?
Anahoji Je, mawakili, na hasa mawakili vijana wana matarajio gani na Rais wa TLS ajaye?, Je, TLS inaweza kujifunza mamnbo gani kutoka Pan African Lawyers Union (PALU) na Black Lawyers Association (BLA)?
Mtatiro anahoji Sera na ujiendeshaji kama huu wa PALU na BLA zinahitaji viongozi gani kuzisukuma kwa muktadha wa TLS? Je, ukiwachambua mawakili wote ambao wanagombea urais wa TLS, ni wagombea gani miongoni mwao wanaonekana wana ushawishi, na kwa nini?
Swali lingine kwa mujibu wa Wakili Mtatiro ni Je, miongoni mwa hawa wenye ushawishi mkubwa, ni nani anaweza kuiongoza TLS kwa mafanikio zaidi kuliko mwenzake? Kwa nini? Na je Misimamo na mitazamo ya washindani wakuu ina tija yoyote ndani ya TLS? Na ni nani anaweza kuiongoza TLS kwa mafanikio zaidi?
Je, TLS inahitaji Rais wa namna gani kwa muktadha wa sasa wa nchi yetu?
Anasema ni wazi kwamba (TLS), kwa sasa kinahitaji Rais ambaye haji kujianzishia tu mambo yake vile atakavyo, kinahitaji Rais ambaye atakuja kuendeleza na kuweka mkazo kwenye mambo muhimu na mazuri (misingi) iliyowekwa na watangulizi wake, yaani Mawakili Profesa Edward Hosea na Harold Sungusia.
Anasema watangulizi hao ambao wamefanya majukumu yao hivi karibuni– pamoja na kurekebisha maeneo ambayo hayakufanyika vizuri, bila kusahau kujenga uwezo wa kuwaunganisha mawakili.
Anasema TLS ni Chama cha kitaaluma kinachohitaji Rais mtendaji, mweledi, mtulivu, mwenye uwezo wa kushawishi wadau wote wa sheria ndani ya nchi, mwenye maono yanayoweza kutekelezeka bila papara.
Mtatiro anasema anahitajika rais wa TLS atakayeweza kuwaunganisha mawakili wote, atakayekua kiungo muhimu kati ya TLS na mdau mkuu ambaye ni Serikali, na ambaye hatogeuka kuwa “msanii na mpiga kelele”, kueneza chuki kwa misingi ya uanaharakati, utofauti wa ufuasi wa vyama vya siasa, mihemko na jazba.
Mtatiro anasema TLS inahitaji mtu mwenye visheni na busara za kutosha, ambaye anaweza kukisaidia Chama cha Mawakili kutekeleza majukumu yake katika hali ya utulivu na ufanyaji maamuzi wa pamoja na wenye tija.
Je, mawakili, na hasa mawakili vijana wana matarajio gani na Rais wa TLS ajaye?
Mtatiro anasema Mawakili vijana, kama ilivyo kada ya vijana dunia nzima, wana matarajio ya kuona mabadiliko ya haraka katika maeneo muhimu wanayoyatarajia. Lakini mawakili hao wanahitaji washauri na waongozi wazuri, wanahitaji kujengewa utulivu na uwezo wa kuyaona masuala katika dhana pana ambayo inaweza kuwajenga na kuwafanya wawe mawakili wa kipekee siku za mbeleni.
Anasema Mawakili vijana wanazo ndoto muhimu, wanayo matamanio ya kuona na wao wanalelewa na kukuzwa ili kufikia mipango yao kwani Mawakili vijana wengi hawana ofisi, wengi wanafungua kampuni za uwakili ambazo zinaongezeka ukubwa kwa hatua sana na wengi wanakata tamaa kwa sababu sekta ya sheria Tanzania na duniani kote imekua sana, imeongeza ushindani wa ndani uliopitiliza na ina changamoto zake
“Kwahiyo changamoto hizi zinapaswa kutatuliwa au kuwekewa misingi itakayopelekea huko tuendako vijana wapya katika taaluma hii muhimu waweze kujisimamia na kusimama wenyewe.
Kimaadili pia, mawakili vijana wanayo dhima na wajibu wa kujifunza maadili na mienendo bora inayokubalika katika utekelezaji wa majukumu yao ya kiuwakili kama inavyoelezwa katika sheria na kanuni mbalimbali za maadili ikiwemo Kanuni za Maadili za Mawakili za Mwaka 2022,” anasema.
Anasema mienendo inayokubalika kwa mawakili vijana inaweza kupatikana kwa kujifunza kupitia matendo mema ya mawakili wazoefu wanaowapokea kwenye ofisi za makampuni ya uwakili na kwamba huko wataweza pia kujifunza zaidi stadi kazi, staha na uadilifu kitaaluma na kuepuka mambo mbalimbali yasiyohitajika kitaaluma ikiwemo kutotumika kwenye shughuli mara mbili (double dealings), hasa kwa wateja wanaowahudumia lakini kutumika pia kisiasa.
Je, TLS inaweza kujifunza kitu kutoka PALU na BLA?
Mtatiro anasema katika kuitafakari TLS, waliona waweke uzoefu wa namna baadhi ya vyama vya mawakili duniani vinavyojiendesha, hasa eneo la kazi zake, utaratibu wa kufanya kazi hizo na wadau wake wakuu.
“Tunaweza kuchukua mifano ya PALU au Black Lawyers Association BLA. Unapofuatilia kwa kina yanayofanyika kwenye vyama hivi unagundua kuwa hivi ni vyama vinavyotoa taswira halisi kuhusiana na kazi kubwa inayofanywa kimkakati na kitaaluma kwenye tasnia ya sheria,” anasema na kuongeza
“Vyama hivi vimekuwa machampioni wa kuweka mkazo katika mabadiliko na masuala ya haki za binadamu na vinafanya kazi nzuri kwa karibu na serikali mbalimbali duniani bila kuviweka mbali vyombo vya haki vya kimataifa kushawishi na kutengeneza miswada inayoweza kuwa sheria kwa ajili ya kukuza haki na usawa duniani,” anasema.
Mtatiro anasema vyama hivi vinatoa msaada wa kisheria kwa uzito kwa jamii ambazo hazijafikiwa ipasavyo na kuondoa matabaka yanayoweza kujitokeza na vinatoa mafunzo na kozi mbalimbali kwa mawakili ili kuwajengea uwezo waweze kufanya kazi zao kitaaluma na kwa mafanikio.
Mtatiro anasema vimekuwa vinaingilia mashauri yenye maslahi mapana ya kitaifa, kuongeza changamoto kwa kukaa chini na serikali na vyombo vya sheria ili kushawishi mabadiliko mbalimbali katika masuala hayo na tasnia ya sheria, kimkakati na kwa utulivu na bila kuvunja uhusiano wake na serikali
“Vyama hivi pia vimekuwa vikifuatilia mwenendo wa demokrasia na utawala bora na kuwaleta wadau mbalimbali wa sheria mezani hasa serikali na vyombo vyake, ili kutatua changamoto zilizoko kwa utulivu na maelewano. Haya yote yamekuwa yakifanywa kwa kuihusisha serikali na vyombo vyake vya kisheria kwa asilimia mia moja,” anasema
“Kwa muktadha huu wa TLS, kunahitajika viongozi wenye ushawishi wa kisera na kimawazo kwa serikali na mahakama, ili viongozi hao wawe na uwanda mpana wa kufanya kazi na mamlaka hizi muhimu na zingine kwa maslahi mapana ya mawakili
“Mstari wa TLS kuelekea mahakamani na serikalini unapokatika au kuyumba, si rahisi mawakili peke yetu na chama chetu kufikia yale malengo tuliyojiwekea, kwani hatuishi ndani ya kisiwa peke yetu,” anasema.
“Je, ukiwachambua mawakili wote wanaogombea nafasi ya kiti cha urais wa TLS, ni nani miongoni mwao wanaoonekana wana ushawishi, kwa nini?
Mwisho
ZINAZOFANANA
Serikali: Sera ya Bima ipo hatua za mwisho kukamilika
Serikali yaipa ITA jukumu la utafiti wa mapato
Benki ya NBC yatambulisha kampeni ya Kilimo Mahususi kwa wakulima na wafugaji Mbeya