November 24, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Serikali yaipongeza Sahara Spark, yawaahidi kuwashika mkono

Dk. Amos Nungu, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi (Costech)

 

SEREKALI imesema kuwa itaendelea kutoa mazingira wezeshi kwa wabunifu na wavumbuzi katika masuala ya Teknolojia ili kuinua na kampuni changa za kibunifu ‘Startup’. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamesemwa leo tarehe 27 Septemba, 2024 na Dk. Amos Nungu, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi (Costech), kwenye onesho la wiki ya Sahara Spark 2024, katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam iliyoandaliwa na Kampuni ya Sahara Spark.

Tukio hilo liliobeba kauli mbiu ya ‘Watu, ujuzi na Ulimwengu mpya’ limewakusanya pamoja wabunifu wa teknolojia, wafanyabiashara pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo na teknolojia na kuwapa fursa ya kushiriki maonesho ya kibiashara pamoja na kujadili maswala mbalimbali ya teknolojia, maendeleo na uchumi.

Dk. Nungu amesema kuwa Tume ya Sayansi itaendelea kuwashika mikono wabunifu na kampuni changa za kibunifu kwa kuwalea ikiwa ni sehemu ya wajibu wa Costech.

‘Matukio kama haya yanawasaidia vijana kuona fursa kama ilivyo kauli mbiu yao ya ‘watu, ujuzi na ulimwengu ujao’ tunahitaji watu wenye ujuzi sahihi weweze kushindana kwa ajili ya ulimwengu ujao,’ alisema Dk. Nungu.

Amesema kuwa Costech inatoa pesa kwa vijana wenye mawazo mazuri ya ubunifu “hiyo pesa tunaiita mbegu halafu baadaye watu kama Sahara Spark wanatafutia fursa zaidi.”

Kwenye onesho hilo mijadala mbalimbali inaendelea leo mpaka kesho tarehe 28 Septemba, 2024 kwenye ukumbi wa Mlimani city.

Mkurugenzi Mtendaji wa Sahara Spark, Jumanne Mtambalike

Kwa kutambua changamoto na pengo lililopo baina ya ujuzi unaohitajika na ule unaopatikana katika soko la ajira, Sahara Sparks inalenga kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuandaa mijadala mbalimbali itakayoongeza ufahamu kuhusu changamoto hiyo na kuleta suluhu za kimkakati ikiwemo kuunda sera zitakazo saidia kutatua changamoto hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Sahara Spark, Jumanne Mtambalike alisema kuwa Sahara Spark imekusudia kuchagiza mijadala mbalimbali itakayoangazia namna gani teknolojia, ubunifu na ujasiliamali unavyosaidia kuongeza ajira na kukuza uchumi wa taifa.

Amesema majadiliano haya yatatilia mkazo zaidi kuhusu rasilimali watu hususani vijana na jinsi ya kuwaandaa kwaajili ya ulimwengu mpya wa ajira.

About The Author