SERIKALI imeipongeza shule ya msingi na sekondari, Green Acres ya jijini Dar es Salaam kwa namna ambavyo imekuwa ikifanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kitaifa kuanzia ngazi ya Wilaya hadi taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Pongezi hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Victor George, wakati wa mahafali ya 24 ya shule hiyo yaliyohusisha wanafunzi wa awali, msingi na sekondari.
“Nawapongeza sana kwa kuendelea kufanya vizuri kitaaluma na nawashauri muendelee kuwekeza kwa wanafunzi hawa maana bila hivyo hatuwezi kuwa na taifa bora la kesho na mmeweka miundombonu mizuri ambayo inawawezesha kusoma kwa utulivu,” alisema.
Alisema serikali ya awamu ya sita imeweka kipaumbele kwenye kuwekeza kwenye ngazi zote za elimu kuanzia awali, msingi sekondari, vyuo vikuu vikuu vya kati ili watoto wanaopata fursa ya kwenda huko kupata elimu bora.
“Vijana huu ni mwanzo tu wa safari ndefu ya maisha, msione mmefika mwisho mnapaswa kuwekaa bidii sana katika masomo yenu kwa hiyo ili mpate mafanikio maishani lazima mhakikishe mnasoma kwa bidii sana,” alisema.
Aliwataka wazazi waendelee kuwa karibu na wanafunzi hao kwa kuhakikisha wanasoma kwa bidii kufikia elimu ya vyuo vikuu ili waweze kufikia ndoto zao.
Alisema amefurahi kuona vipaji mbalimbali vilivyoonyeshwa na wanafunzi wa shule hiyo kwenye maonyesho ya kitaaluma hali inayoonyesha kwamba walimu wa shule hiyo wamefanyakazi kubwa kuwaandaa.
“Hata matokeo yenu ya kuanzia shule ya msingi na sekondari yamekuwa mazuri mwaka hadi mwaka nawapongeza sana mmekuwa mkifanya vizuri kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa na Kitaifa msibweteke endeeni kufanya vizuri zaidi,” alisema
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Green Acres, John Pinda alisema wanafunzi wa shule hiyo kuanzia awali, msingi na sekondari wameandaliwa vizuri na wanatarajiwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya kitaifa.
Alisema wamefanikiwa kutengeneza chumba cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA, maktaba kubwa ya kisasa, uwanja wa kisasa yote hiyo katika kuongeza mnyororo wa thamani wa elimu na kwamba wanaimani kuwa hata mitihani ya kitaifa ya darasa la saba na kidato cha nne mwaka huu watafanya vizuri sama.
“Wizara imeelekeza kila shule iwe na darasa la TEHAMA sisi tumeshakamilisha kwasababu tunataka wanafunzi wawe na uwezo wa kujua masuala mbalimbali ya teknolojia ya kisasa duniani kwa hiyo tunakwenda na wakati,” alisema.
ZINAZOFANANA
Wazazi wapewa angalizo matumizi ya simu, kompyuta kwa watoto
Watumishi CBE wahimizwa kuishi kwa upendo
TCU yafungua dirisha jipya udahili elimu ya juu