NBC yaitambulisha “NBC Shambani” kwa wakulima wa Songwe
BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua rasmi kampeni yake ya “Wekeza NBC Shambani Ushinde” mkoani Songwe, ikiwa ni hatua mahsusi ya kuwawezesha wakulima wa mazao mbalimbali ikiwemo kahawa na ufuta kupitia huduma jumuishi za kifedha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Songwe … (endelea).
Sambamba na uzinduzi huo, uongozi wa mkoa pamoja na wakulima wametoa wito kwa benki hiyo kufungua tawi jipya katika mji wa Mlowo, wilayani Mbozi, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha na kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo.
Uzinduzi huo ulifanyika jana Mlowo, Mbozi, ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega, ukihusisha wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo wakiwemo viongozi wa vyama vya msingi na vyama vikuu vya ushirika (AMCOS), pamoja na washiriki wa mnyororo wa thamani wa kilimo.
Kwa upande wa NBC, Mkuu wa Bidhaa na Mauzo, Abel Kaseko, aliongoza ujumbe wa benki hiyo katika hafla hiyo, akieleza kuwa kampeni hiyo ya miezi minne inalenga kuwahamasisha wakulima kutumia huduma rasmi za kifedha huku wakipata fursa ya kushinda zawadi mbalimbali, zikiwemo pikipiki na kompyuta mpakato (laptop).
Akizungumza katika hafla hiyo, Mbega aliipongeza NBC kwa juhudi zake za kuendeleza sekta ya kilimo kupitia ubunifu wa huduma za kifedha zinazolenga wakulima na wafugaji. Alisisitiza kuwa kampeni hiyo ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa wakulima, hususan kupitia elimu ya fedha, huduma rafiki za mikopo na bima za afya na kilimo.

“Takribani asilimia 80 ya mapato ya Wilaya ya Mbozi yanatokana na kilimo. Hivyo, tunathamini jitihada zote zinazolenga kuwawezesha wakulima wetu. Kampeni hii ya NBC ina upekee kwa kuzingatia pia elimu ya nidhamu ya fedha, ambayo itawajengea wakulima uwezo wa kuweka akiba, kutumia bima na kuwekeza katika kilimo cha kisasa,” alisema.
Aliongeza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza imani ya wakulima katika taasisi rasmi za kifedha na hivyo kuchochea uchumi jumuishi, akilinganisha na miaka ya nyuma ambapo wakulima wengi walikosa uaminifu mbele ya taasisi hizo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa dhamana.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuiomba NBC kufungua tawi katika mji wa Mlowo ili kupunguza adha ya wakulima kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kibenki katika miji ya Tunduma na Mbeya Mjini.
Akifafanua zaidi, Kaseko alisema kampeni hiyo inalenga wakulima wa kahawa na ufuta kupitia vyama vya ushirika na wakulima binafsi wanaohudumiwa na benki hiyo. Ili kushiriki na kupata nafasi ya kushinda zawadi, wakulima wanatakiwa kufungua akaunti ya NBC Shambani na kupitisha miamala yao kupitia akaunti hiyo.

“Sekta ya kilimo inaajiri takribani asilimia 65 ya Watanzania. Ndiyo maana NBC tunaendelea kubuni suluhisho bunifu zinazolenga kuimarisha sekta hii. Kupitia kampeni hii, tunahamasisha matumizi ya mifumo rasmi ya kifedha, huku zawadi zikiwa ni kichocheo cha kuongeza ushiriki wa wakulima,” alieleza.
Kwa upande wao, wakulima akiwemo Bw. George Mwashilanga, Nickson Dirisha, na Hifadhi Anderson Mdono, walieleza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakikumbwa na changamoto za gharama za uendeshaji wa akaunti pamoja na kufungwa kwa akaunti zisizotumika, hali iliyodhoofisha imani yao kwa taasisi za kifedha.
Hata hivyo, walipongeza akaunti ya NBC Shambani kwa kutokuwa na makato ya uendeshaji na kutofungwa kirahisi, wakisema ni suluhisho linaloendana na mahitaji halisi ya wakulima.
“Hii ni fursa kubwa kwetu. Akaunti hii haina makato na haitofungwa kirahisi. Tuko tayari kuwa mabalozi wa kuhamasisha wakulima wengine kujiunga na NBC Shambani,” alisema Bw. Mwashilanga, huku pia akisisitiza umuhimu wa kufunguliwa kwa tawi la NBC Mlowo.