Chadema yaahidi kuendeleza urithi wa waasisi wake kufikia madaraka kwa njia ya demokrasia
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche amesema chama hicho kimejipanga kulinda heshima na imani ya waasisi wake kwa kuhakikisha kinafikia lengo la kushinda mamlaka ya nchi kupitia njia ya kidemokrasia.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Heche ameyasema hayo akiwa katika viunga vya Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe mara baada ya ibada ya kumuaga aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu (Bara), Medard Mutungi, ambapo viongozi na wanachama wa Chadema walijumuika kutoa heshima za mwisho.
Amesema kifo cha Mutungi ni pigo kubwa kwa chama hicho, hasa ikizingatiwa kuwa kimekuja muda mfupi baada ya kuondokewa na mmoja wa waasisi wake, Edwin Mtei, ambaye alikuwa miongoni mwa watu waliopigania kuanzishwa kwa chama hicho.

“Katika mwaka mmoja huu tumepoteza waasisi wawili wakubwa; Mzee Mtei na Mutungi. Hii inaonyesha historia ya chama chetu kilichoanzishwa na watu waliokuwa na maono ya mabadiliko,” alisema Heche.
Kutokana na msiba huo, Heche amesema Chadema imeahirisha vikao vya Kamati Kuu vilivyokuwa vikiendelea ili kutoa nafasi kwa viongozi kushiriki kikamilifu katika shughuli za mazishi.
Ameongeza kuwa viongozi waliopo sasa wamepewa dhamana ya kuendeleza malengo ya waasisi wa chama hicho, hususan kuhakikisha Chadema inafikia lengo lake la kushika madaraka ya nchi kupitia njia za kidemokrasia.
Heche amehitimisha kwa kutoa pole kwa familia ya marehemu Mutungi pamoja na wanachama wote wa Chadema, akimtakia marehemu mapumziko ya amani.