BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imezindua rasmi utekelezaji wa mpango wa ufadhili wa masomo ya ufundi kwa vijana nchini unaofahamika kama “NBC Wajibika Scholarship”. Mpango huu ni sehemu ya juhudi endelevu za taasisi hizo mbili katika kuunga mkono azma ya serikali ya kukuza ajira, hasa kwa vijana, na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea). Uzinduzi huo umefanyika katika Makao Makuu ya NBC jijini Dar es Salaam, ukihudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka pande zote mbili, wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore. Akizungumza katika hafla hiyo, Sabi alisema kuwa katika hatua ya awali, NBC imetenga jumla ya shilingi milioni 150 kufadhili wanafunzi 588 watakaopatiwa mafunzo ya muda mfupi katika fani mbalimbali za ufundi. Fani hizo ni pamoja na umeme, uhandisi mitambo, ujenzi, pamoja na huduma za hoteli na utalii—sekta ambazo zina mchango mkubwa katika ajira na uchumi wa nchi. Alifafanua kuwa mafunzo hayo yatadumu kati ya miezi mitatu hadi sita na yatatolewa katika vyuo vya VETA vilivyopo Morogoro (Kihonda) na Mwanza. Aidha, kila mwanafunzi atafunguliwa akaunti ya “NBC Kua Nasi” ili kuwaunganisha na mfumo rasmi wa kifedha, sambamba na kuwapatia fursa za kukuza ujuzi wa kibiashara kupitia majukwaa ya NBC Business Club. “Kupitia mpango huu, hatulengi kuwapatia vijana vyeti pekee, bali tunawaandaa kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa taifa. Tunaamini uwekezaji huu utasaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana, ambao kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wako chini ya umri wa miaka 35,” alisisitiza Sabi. Kwa upande wake, Kasore aliipongeza NBC kwa hatua hiyo, akieleza kuwa ufadhili huo utachangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha malengo ya VETA ya kutoa mafunzo kwa wanafunzi 120,000 kila mwaka. Alibainisha kuwa hadi sasa taasisi hiyo imefanikiwa kusajili wanafunzi zaidi ya 101,000, hivyo mpango huo unakuja wakati muafaka. “Hatua hii ya NBC kufadhili wanafunzi 588 ni mchango mkubwa katika safari yetu ya kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata ujuzi wa kujiajiri na kuajirika. Tunatoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano huu, kwani uwekezaji katika elimu ya ufundi ni uwekezaji wa moja kwa moja kwa maendeleo ya jamii,” alisema Kasore. Aidha, alieleza kuwa uteuzi wa mikoa ya Morogoro na Mwanza kwa awamu ya kwanza umezingatia mahitaji ya wataalamu katika maeneo hayo, huku akibainisha kuwa hatua inayofuata ni utekelezaji kamili wa mpango huo na uwezekano wa kuupanua katika maeneo mengine nchini. “Kwa ujumla, uzinduzi wa NBC Wajibika Scholarship unaashiria hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na taasisi za umma katika kujenga nguvu kazi yenye ujuzi, inayoweza kukabiliana na changamoto za soko la ajira na kuchochea maendeleo jumuishi ya taifa,’’ alihitimisha. Share this… Facebook Pinterest Twitter Linkedin Whatsapp About The Author Erasto Masalu See author's posts Post navigation Hadithi ya ushindi inaanza na wewe ukiingia kwenye Vita Ya Kifalme