Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chadema akiwa mahakamani
IKIWA ni siku 286, miezi tisa akiwa anasota kwenye gereza Kuu la Ukonga, Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), leo ikiwa ni siku ya kumbukizi ya siku yake ya kuzaliwa. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Tundu Lissu ni mwanasiasa maarufu nchini Tanzania, anayejulikana kwa ujasiri wake katika kupambana na ufisadi na ukiukaji wa haki za binadamu.
Tundu Antiphas Mughwai Lissu alizaliwa tarehe 20 Januari 1968 katika wilaya ya Ikungi, mkoani Singida. Alisoma shule ya msingi Mahambe na baadaye kujiunga na shule ya sekondari ya Ilboru, Arusha, ambapo alihitimu mwaka 1983. Lissu alisomea sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na kujiunga na harakati za kisiasa akiwa na umri mdogo.
Tundu Lissu alifaulu mtihani wa darasa la saba na kwenda shule ya sekondari ya Ilboru, Arusha. Shuleni hapo, yeye ndie aliyekuwa mwanafunzi mdogo kuliko wote. Licha ya udogo wake, alikuwa mwiba mkali kwa prefects na walimu. Akiwa kidato cha tatu wenzake walimtaka awe prefect lakini alikataa kwani alizoea kuwaita “manyoka” kwa tabia yao ya kupenda kupeleka taarifa za wanafunzi kwa walimu.
Tundu Lissu alifaulu vizuri na kuingia kidato cha tano shule ya sekondari ya Galanosi, Tanga. Akiwa Galanosi, akapewa Uenyekiti wa Kamati ya Taaluma. Hata hivyo, akakorofishana vibaya mno na mwalimu wa taaluma na kuvuliwa cheo hicho.

Akiwa kidato cha sita mwaka 1988, kulikuwa na disko la graduation. Kidato cha sita wakaruhusiwa kwenda kucheza na Korogwe girls lakini kidato cha nne wakakataliwa na wakaambiwa wataletewa taarabu shuleni hapo. Lissu aliona huo ni uonevu na daima shuleni hapo alichukia mno mwanafunzi mwenzake kuonewa hata kama ni wa madarasa ya chini. Hivyo, akaandika Waraka “TAARAB FOR WHOSE INTEREST”.
Lissu hakuandika jina lake kwenye waraka huo. Akaubandika kwenye ubao wa matangazo usiku. Walimu walipouona walichukia sana na wakachunguza na kuhisi mwanafunzi pekee aliyepinda shuleni hapo mwenye ubavu wa kuandika vitu kama vile ni Lissu tu hivyo wakamkamata. Walimu wakamwita Lissu mchochezi na hivyo akapewa suspension. Hata hivyo, baadae akarudishwa shuleni na kisha akafanya mtihani wa kidato cha sita.
Mwaka 1989 akaenda Mafinga JKT kisha Itende JKT kwa mwaka mmoja. Wakati huo, vuguvugu la vyama vingi lilikua limepamba moto nchini huku CCM ikiwa haitaki kabisa kuskia mambo ya vyama vingi. Katiba ya CCM ilikuwa inautambua Mkoa wa Majeshi hivyo ilituma viongozi wake kutembelea kambi zote na kuulezea msimamo wa CCM kutotaka kuskia takataka inayoitwa vyama vingi.

RPC Omary Mahita (Rukwa) na Kanali wa Andrew Shija wakitokea Mkoa huo wa Majeshi wakapangiwa kwenda Itende JKT kuwaelezea servicemen msimamo wa chama. Walipofika wakaitisha mkutano mkubwa na ukumbi ukawa umefurika. Katika mkutano huo, Mahita na Shija wakaeleza kwamba “Sisi haya mambo ya vyama vingi hayatuhusu. Haya ni mambo ya wazungu huko Ulaya mashariki hivyo tusiyashabikie”.
Kitu ambacho viongozi hao hawakukijua ni kwamba miongoni mwa servicemen hao alikuwepo kijana mmoja very brilliant mwenye uelewa mkubwa wa mambo mengi yanayoendelea duniani asiye na simile kuongea kilichomo akilini mwake.
Lissu alikuwa ameskiliza hotuba ya Baba wa Taifa alipoongea na Baraza Kuu la Umoja wa vijana wa CCM Mwanza wiki chache kabla ya mkutano huo wa akina RPC Mahita. Mwalimu alikuwa amesema -“Wanaodhani mageuzi hayatuhusu bali yanazihusu nchi za Ulaya mashariki pekee ni wajinga kwani Tanzania sio kisiwa”.
Muda wa maswali ulipofika huku wengi wakiamini hakuna atakaekuwa na ubavu wa kuuliza swali, Lissu bila kuogopa na kwa ujasili wa hali ya juu ambao haukuwahi kuonekana hapo Itende JKT, akanyoosha mkono. Servicemen wenzake waliokuwa wakijua misimamo yake isiyoyumba walijitahidi kumshusha mkono bila mafanikio.
Huku akitumia lugha kali bila kumun’gunya maneno kama kawaida yake, Lissu aliwauliza viongozi hao -“Je, mjinga ni Baba wa Taifa aliyesema mageuzi ya vyama vingi yanatuhusu au ni nyie mnaosema hayatuhusu?”
RPC Mahita, kwa wajihi, ni mweupe sana lakini swali hilo lilimbadilisha na kuwa mwekunduuuu. Ghafla bin vuu maafande wakamkimbilia Lissu kutaka kumkwida kwa “kosa” la kutukana meza kuu. Bahati nzuri, Kanali Shija akawa na busara na akawazuia na kuwaambia “Huyo kijana Lissu yupo sahihi kwani hicho ndicho alichosema Baba wa Taifa.” Huo ndio ukawa mwisho wa mkutano.

Baada ya songombingo na tafrani hiyo ya kipekee siku hiyo , maafande wote wa Itende JKT wakaanza kumuogopa sana Lissu wakiamini yeye ni mtu wa Usalama wa Taifa na akawa hapangiwi tena kazi bali akawa anakula shushi hadi kumaliza muda wake!
Kutokana na kufaulu vizuri kidato cha sita, Lissu alijiunga na kitivo cha sheria mwaka 1991 UDSM. Huko aliendelea na harakati zake za kupigania haki za wanafunzi na akajiunga na NCCR MAGEUZI. Miaka hiyo, chama hicho kilichokuwa chini ya mmoja ya viongozi waliowahi pendwa mno nchini, Mh. Augustin Mrema, ndicho kilikuwa chama kikuu cha upinzani nchini.
Baadae mwaka 1995, Lissu akaenda kusomea shahada ya uzamili chuo cha Warwick UK. Alipofika huko akaomba ruhusa aje kugombea ubunge Singida mashariki. Hata hivyo, kutokana na maandalizi duni, kura hazikutosha hivyo akarejea masomoni.
Lissu alipomaliza masomo yake 1997 alirejea na kufanya kazi ya sheria Arusha. Baadae akaoa na kuhamia Dar es Salaam. Akawa mmoja wa wanasheria wa chama cha wanasheria wa mazingira (LEAT) pamoja na Dk. Rugemeleza Nshalla na Alex Shauri.
Lissu alikuwa Mbunge wa Singida Mashariki kupitia chama cha upinzani, CHADEMA, kuanzia mwaka 2010 hadi 2020. Katika kipindi chake cha ubunge, alijulikana kwa kupambana na ufisadi na kutoa sauti yake dhidi ya serikali, hasa wakati wa utawala wa Rais John Magufuli. Alikuwa pia Mwenyekiti wa CHADEMA kuanzia Januari 2025.
Katika mwaka 2017, Lissu alinusurika jaribio la mauaji baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 16 mjini Dodoma. Tukio hili lilizua maswali mengi kuhusu usalama wa wanasiasa wa upinzani nchini Tanzania. Baada ya matibabu ya muda mrefu nchini Kenya na baadaye Ubelgiji, Lissu alirejea Tanzania mwaka 2020 na kugombea urais kupitia CHADEMA, ingawa hakushinda.
Lissu amekuwa sauti muhimu katika harakati za kudai demokrasia, utawala wa sheria, na haki za kiraia nchini Tanzania. Anajulikana kwa ujasiri wake wa kukosoa serikali na kuhamasisha umma kuhusu masuala ya haki na uwazi.
Kwa ujumla, Tundu Lissu ni mfano wa ujasiri na kujitolea katika siasa za Tanzania, na mchango wake utaendelea kuwa muhimu katika historia ya nchi
HAPPY BIRTHDAY LISSU, HAPPY BIRTHDAY TUNDU LISSU, HAPPY BIRTHDAY MWAMBA
ZINAZOFANANA
AG Zanzibar aweka mapingamizi kesi za Uwakilishi
Butiku aita Wazee kujadili ya 29 Oktoba
Tume.yamtangaza Museven mshindi Urais Uganda