January 20, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Butiku aita Wazee kujadili ya 29 Oktoba

 

MWENYEKITI Mtendaji wa Mfuko wa Mwalimu Julius Nyerere – The Mwalimu Nyerere Foundation (MNF), Joseph Butiku, amesema, taasis hiyo, imeitisha mkutano mahususi wa kuzungumzia Haki, Amani na maendeleo nchini Tanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza leo Jumatatu, tarehe 19 Januari 2026, ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Butiku amesema, mkutano huo, utafanyika Alhamisi wiki hii.

Amesema, mkutano huo umeandaliwa kwa lengo la kutoa nafasi kwa wazee wenye hekima kujadili na kutoa maoni yao kuhusu misingi iliyoundwa na kudumisha Taifa kuwa nchi ya amani, umoja, haki na yenye matumaini ya maendeleo endelevu.

Butiku ametaja sababu za kufanyika kwa kikao hicho, ni matukio ya ghasia yaliyotokea tarehe 29 Oktoba 2025, wakati wa uchaguzi mkuu.

Mkutano uliyoitishwa na Butiku unafanyika wakati Rais Samia Suluhu Hassan, ameunda Tume ya uchunguzi wa matukio ya 29 Oktoba mwaka jana na ikiwa bado haijamaliza kazi yake.

Tume ya Rais, inaongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Othuman Chande Othuman.

Aidha, mkutano wa Butiku umeitishwa wakati Rais Samia akieleza kuwa serikali yake, haitalazimishwa kufanya maridhiano kwa matakwa ya kundi fulani.

Akizungumza na wanaoitwa, “Wazee wa Dar es Salaam,” Desemba mwaka jana, Rais Samia alisema, kuna watu wanatoa masharti kwamba ili waingie kwenye mazungumzo ya maridhiano, ni sharti aliyeko gerezani aachiwe huru.

Akaongeza, “Sitapokea masharti kutoka kwa yoyote.” Rais hakumtaja aliyeko gerezani ambaye anashinikizwa kumuachia huru kwanza kabla ya kuingia kwenye mazungumzo ya maridhiano. Wala hakumtaja aliyetoa sharti hilo.

Hata hivyo, kiongozi wa upinzani anayefahamika kuzuiliwa gerezani, ni Tundu Lissu, mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo na aliyenukuliwa akisema, “hatutaingia kwenye mazungumzo ya maridhiano bila Lissu kuwa huru,” ni John Heche, makamu mwenyekiti wa chama hicho.

Kwa mujibu wa Butiku, matukio ya Oktoba mwaka jana, yameibua haja ya kutafakari kwa kina misingi ya amani na umoja iliyojengwa tangu enzi za waasisi wa taifa, ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa na mshikamano na mwelekeo wa maendeleo endelevu.

Amesema mkutano huo unalenga kuwapa wazee nafasi ya kutoa mawazo na mapendekezo yao kwa kutumia busara na uzoefu waliopata kwa miaka mingi, ili kuendeleza maadili ya amani, haki na utulivu wa kisiasa.

Mwenyekiti huyo ameweka wazi kuwa mazungumzo ni nyenzo ya upatanishi na utatuzi wa migogoro, hivyo ni muhimu kuwa na majadiliano ya kina kwa lengo la kuimarisha amani na kuzuia migogoro ya kisiasa kuibua vurugu zitakazoharibu maendeleo ya taifa.

Matukio ya 29 Oktoba 2025, yaliyosababisha mauaji ya raia, yalitokana na hatua ya serikali ya kukabiliana na waandamanaji wasiokuwa na silaha, ambako maelfu ya watu wanahofiwa kufariki dunia.

Mpaka sasa, serikali haijatoa idadi kamili ya watu waliouawa katika maandamano hayo na haijaeleza mahali iliko miili ya waliouawa.

Naye Butiku hajataja majina ya wazee watakaohudhuria mkutano wake, ingawa taarifa zinasema, baadhi ya viongozi wa madhehebu ya kidini, wameamua kujitenga na mkutano huo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kidini wenye ushawishi mkubwa, vuongozi hao wanadai kuwa “serikali haijaonyesha utayari wa maridhiano.”

“Baadhi ya viongozi wa kidini, wanatilia mashaka kasi ya Butiku katika jambo hili. Kuna watu wanamuona kama anafanya kazi kwa msukumo fulani, ndio maana wengi wameamua kujitenga,” anaeleza kiongozi mmoja wa kidini aliyealikwa mkutano huo, lakini amegoma kuhudhuria.

Ameongeza, “Kuna wengine wamemuambia watatuma uwakilishi kwa kuwa wamebanwa na ratiba. Siyo kwamba hawawezi kufika, ni kwa sababu, wameona anakwenda mbio, wakati Tume ya Rais, haijamaliza kazi yake.”

About The Author

error: Content is protected !!