James Mbowe
JAMES Mbowe, mtoto wa aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kwa takribani miaka 20, ameomba radhi kwa kujiunga na Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA). Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Kwa mujibu wake, amejutia uamuzi wake wa kuondoka Chadema – chama anachodai kimemlea na kumkuza – na kukimbilia Chaumma. Amedai kuwa kuna siku atafichua siri ya kilichomsababisha kujiunga na Chaumma.
James ametoa kauli hiyo, leo tarehe 8 Januari 2026, katika taarifa yake kupitia mitandao ya kijamii.
Akiongeza kuwa suala la yeye kuondoka Chadema, liliwaumiza watu wengi na hivyo kutumia nafadi hiyo kuwaomba radhi wale walioumia.
James alitangaza kujiunga na Chaumma tarehe 6 Agosti 2025, akiwa na Yeriko Nyerere, makao makuu ya Chaumma, Kinondoni, Dar es salaam.
Hata hivyo, mara baada ya kumalizika uchaguzi mkuu wa Chadema, Januari mwaka jana, mamia ya waliokuwa wafuasi wa Mbowe, wakiongozwa na John Mrema, Salum Mwalimu, Benson Kigaila na Catheren Ruge, walianza kuondoka chama hicho na kujiunga na Chaumma.

Katika maeleo yao, wafuasi hao wa Mbowe, walidai kuwa wanaondoka Chadema baada ya chama hicho, kukosa uongozi thabiti wa kuwapeleka mbele, ingawa wachambuzi wanasema, “walitumika na watawala kuidhoofisha uongozi mpya.
Kwenye uchaguzi huo, uliokuwa huru na haki, Mbowe alishindwa na Tundu Lissu na tangu wakati huo, amejitenga na Chadema, huku akidaiwa kuunga mkono wafuasi wake kukimbilia Chaumma.
Taarifa mikononi mwa MwanaHALISI Online, zinaeleza kuwa kuondoka kwa James Mbowe, ndani ya Chaumma, ni sehemu ya mkakati mahususi unaopikwa ili kumsafishia njia Mbowe ya kurejea Chadema na kuvuruga uongozi mpya.
Bali kiongozi mmoja wa chama hicho, amemueleza mwandishi wa gazeti hili, kwamba mkakati huo hautafanikiwa kwa kuwa “…wananchi wameshamfahamu Mbowe kuwa amelambishwa asali, ili kuibeba CCM (Chama Cha Mapinduzi).
“Nani anamuamini Mbowe leo? Hata wale waliokuwa bado wanamuamini ndani ya Chadema, wengi wao sasa, hawamkubali tena.

“Hiki chama kinapita kwenye nyakati ngumu sana. Huyu angekuwa mwenzetu, asingejitenga nacho. Kimya chake, kinathibitisha kuwa siyo mwenzetu, hivyo hawezi kufanya kazi aliyotumwa,” ameeleza.
Anaongeza, “Mbowe, aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema, kwa miaka 21, amejijengea taswira mbaya tokea Januari mwaka jana, aliposhindwa kutetea wadhifa wake wa uenyekiti. Wengi wanamuona sasa, kuwa ni mbinafsi, amesheheni visasi, chuki, msaliti na msahaulifu.”
Anasema, baada ya kushindwa uchaguzi, Mbowe alisema ameridhika na mchakato ulivyokwenda, ingawa akaeleza kuwa mchakato wa kampeni umeacha majeraha na kuwataka waliochaguliwa kuyatibu kwa kuleta maridhiano.
“Lakini yeye akawa wa kwanza, kukimbia maridhiano. Akaanza kutuma watu wake, kukiumiza chama kwa kufungua mashauri mahakamani na wengine kuwapeleka Chaumma,” anafafanua.
ZINAZOFANANA
Hesabu zakataa ushindi wa CCM
Watu 100 wameuawawa shambulio la kukamatwa Maduro
Kiongozi wa kijeshi Burkina Faso anusuruka kuuawa