WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Juma Homera, amezindua kliniki ya huduma za msaada wa kisheria (Legal Aid Clinic) mkoani Morogoro, itakayotoa huduma za ushauri na msaada wa kisheria bila malipo kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa serikali wa kusogeza huduma karibu na wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa kliniki hiyo ya siku mbili, Dk. Homera amewataka wananchi kuchangamkia huduma hiyo ya kliniki kwani fursa pekee ya kuwahudumia wananchi wenye migogoro mbalimbali ikiwemo ya ndoa, ardhi, mirathi na ukatili wa kijinsia.
Huduma zitakazotolewa ni pamoja na uwakili, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), huduma za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), pamoja na utoaji wa elimu ya kisheria.
“Kliniki hii inadhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt Rais Samia Suluhu Hassan ya kusogeza huduma za haki karibu na wananchi na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma,” alisema Dkt. Homera.
Aidha, Waziri Homera alizitaka taasisi na mashirika yanayotoa huduma za msaada wa kisheria pamoja na wasaidizi wa kisheria kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa kliniki hiyo, ili kuendelea kuiunga mkono Serikali katika juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa mujibu wa sheria.
Alisema Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kuratibu, kusimamia na kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za msaada wa kisheria ili kuhakikisha wananchi, hususan wale walioko pembezoni, wanafikia haki kwa wakati.

Dk. Homera aliongeza kuwa awamu ya kwanza ya Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria imepata mafanikio makubwa, ambapo jumla ya wananchi 3,734,157 walifikiwa, wakiwemo wanaume 1,807,440 na wanawake 1,926,717, na kupatiwa elimu kuhusu masuala ya sheria, haki za binadamu, utawala bora pamoja na huduma za msaada wa kisheria.
Katika hatua nyingine, Waziri Homera aliipongeza RITA kwa kazi nzuri wanayoifanya, ikiwemo utoaji wa vyeti vya kuzaliwa na utatuzi wa migogoro ya mirathi na ndoa.
Hata hivyo, alisema bado changamoto ya ukatili wa kijinsia inaendelea kuwepo, hivyo Serikali imejipanga kuimarisha huduma za ushauri wa kisheria na unasihi kwa waathirika na manusura wa ukatili huo, pamoja na kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, aliipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kupitia taasisi zake kwa kuleta huduma hiyo mkoani humo, na kuwataka wakazi wa Morogoro kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Stendi ya Zamani ili kunufaika na huduma hizo bila gharama yoyote.
“Nawaomba wananchi wa Mkoa wa Morogoro mjitokeze kwa wingi kuchangamkia fursa hii ili kutatua changamoto zenu zinazohitaji msaada wa kisheria,” alisisitiza RC Malima.

RC Malima pia aliomba Wizara kuzingatia ukubwa wa Mkoa wa Morogoro wakati wa utoaji wa huduma hizo, ambapo alipendekeza kliniki za msaada wa kisheria ziwafikie pia wananchi wa maeneo ya mbali, ikiwemo Ifakara, ili kuwapunguzia usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo Morogoro mjini.
Naye Naibu Kabidhi Wasihi Mkuu wa RITA, Irene Lesulie, alisema cheti cha kuzaliwa ni haki ya msingi kwa kila mwananchi, na kuwasihi wananchi kutumia fursa hiyo kwa kutembelea banda la RITA ili kupata huduma mbalimbali ikiwemo vyeti vya kuzaliwa na masuala ya mirathi.
“Uhitaji wa vyeti vya kuzaliwa ni mkubwa. Kutokana na hali hiyo, RITA kupitia mfumo wa kidijitali wa e-RITA imejipanga kikamilifu kuhakikisha Watanzania wote wanafikiwa,” alisema Bi. Lesulie.
Kwa upande wake, Faudhia Saidi, mkazi wa Kichangani mkoani Morogoro, alisema amenufaika na huduma za RITA baada ya kupatiwa cheti cha kuzaliwa kwa haraka, na kuwahamasisha wananchi wengine wasio na vyeti hivyo kujitokeza kwa wingi.
“Sikuamini kama ningepatiwa cheti changu cha kuzaliwa ndani ya muda mfupi. Nilidhani ingechukua muda mrefu kukifuatilia,” alisema Faudhia.
Kliniki hiyo ya msaada wa kisheria inashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mawakili wa Serikali, Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia, pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, ikiwa na lengo la kutatua changamoto za kisheria zinazowakabili wananchi.
ZINAZOFANANA
AG-SMT ageuzia kibao wapinga ubunge, ahoji Mahkama ya Z’bar
Bagonza achambua wanaopinga Kanisa Katoliki
Maduro afikishwa mahakamani Marekani