February 2, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

AG-SMT ageuzia kibao wapinga ubunge, ahoji Mahkama ya Z’bar

BAADA ya kuzuiwa kutumia wanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar {SMZ}, katika kesi zinazohusu uchaguzi wa wabunge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano {SMT} amekuja kivingine, akihoji mamlaka iliyonayo Mahkama Kuu ya Zanzibar kwenye mashauri hayo. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Mbele ya Jaji Haji Suleiman Haji, jopo la mawakili wanaomwakilisha Mwanasheria Mkuu huyo ambaye ni mmoja wa walalamikiwa kwenye kesi zinazohusu matokeo ya uchaguzi wa ubunge Zanzibar, limeeleza kuwa lina tatizo na “uwezo wa kisheria” wa Mahkama ya Zanzibar na lingependa suala hilo liamuliwe sasa.

Wakati mwanajopo Nalindwa Emmanuel akiwasilisha hoja hiyo leo, mbele ya Mahkama palikuwa na ombi la walalamikaji – wagombea ubunge wa majimbo 19 ya kisiwani Unguja, wote wakiwa ni wanachama wa Chama cha ACT Wazalendo – kutaka waondolewe sharti la kulipa gharama za kesi walizofungua.

Matarajio ya walalamikaji hao yalikuwa watasikilizwa na mahkama, kwa vile wakili anayewawakilisha, Omar Said Shaaban, alishaomba na kukubaliwa kuwa ombi hilo lingesikilizwa leo, baada ya uamuzi mdogo uliohusu hoja yake yeye ya kukataa uwakilishi wa wanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa SMZ.

Na kweli, hoja yake ikasihi. Jaji Haji akisoma uamuzi huo mbele ya hadhara ya wananchi, wakiwemo wana ACT waliofika kushuhudia maendeleo ya mashauri yao, alisema imethibiti kuwa sababu zilizotolewa na wakili wao amekuta zina msingi wa kisheria na kikatiba.

Kwamba, ni kweli Ibara ya 59 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya mwaka 1977, iliyoanzisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa SMT, pamoja na kubainisha majukumu yake, inapotamka wanaofaa kumwakilisha mtendaji huyo popote pale ambapo masuala ya kisheria yanahusika kusimamiwa, Mwanasheria Mkuu wa SMZ hatajwi.

Jaji Haji pia alikiri kuwa hata pale Mwanasheria Mkuu huyo wa SMZ aliposhiriki kwenye Mahkama Kuu wakati wa shauri maarufu la Jina Khatibu Haji dhidi ya Juma Suleiman Nhunga, la mwaka 1987, ilitokana na kualikwa na Mahkama afike na kutoa maoni yake kwa nafasi ya kuwa “rafiki wa Mahkama” na sio kama mwakilishi mahsusi wa wale waliokuwa wakilalamikiwa kwenye rufani.

Kadhalika, alisema anatambua ukweli kuwa mwanasheria mkuu wa SMZ hakuwasilisha ombi rasmi kama inavyotakiwa ikibidi ameona haja, la kutaka kujiunga na mashauri hayo kwa ile hoja waliyoitoa mawakili wa walalamikiwa kuwa “Mwanasheria Mkuu wa SMZ ana maslahi makubwa katika kesi hizi za ubunge kwa vile zinahusu uchaguzi uliofanyika Zanzibar na kushirikisha wananchi wa Zanzibar ambao kisheria yeye anawajibu wa kuwawakilisha ili kulinda na kuyasimamia maslahi yao.”

Upande huo ulijenga hoja hizo kwa kudai msingi wake ni Kifungu Namb 15(1) na (3) cha Sheria Namb 6 cha Sheria ya Kuanzisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar na Utekelezaji wa Majukumu yake. Sheria hiyo ilifutwa na sheria mpya ya mwaka 2013 iliyoanzisha ofisi hiyo.

Jaji Haji akahitimisha uamuzi: “Nazingatia hoja za kisheria alizotoa wakili Shaaban wa upande wa walalamikaji. Sasa ni uamuzi wa mahkama hii kuwa kuwepo kwao kama wawakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa SMT, si halali.”

Wanasheria waliotambulishwa siku ya kutajwa kwa kesi za ubunge, walikuwa Said Salim Said, Mbarouk Suleiman Othman wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa SMZ, na Ali Issa Abdalla aliyetambulishwa kutoka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Wote walikuwepo mahkamani leo wakati uamuzi mdogo ukitolewa, jopo la wanasheria waliotoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa SMT likiongozwa na Wakili Mkuu wa Mashtaka Allan Shija na Nalindwa, wakili mwandamizi.

Kama hiyo haitoshi, upande wa walalamikiwa, ikiwemo pia Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania {INEC} na wasimamizi wa uchaguzi majimboni, walishakataliwa kushirikisha wanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa SMZ.

Kutokana na hoja mpya iliyoibuliwa na upande huo, na kutolewa rai kuwa si busara kusikiliza ombi la walalamikaji la kuhusu kuondolewa malipo ya gharama za kesi, Jaji Haji aliamua kuwa anaakhirisha kesi na kuja kutoa uamuzi mdogo kuhusu hoja hiyo hapo tarehe 14 Januari 2026.

Alikubali ombi la pande zote kwamba atakapokuja kusikiliza ombi hilo linalohusu gharama, mahkama itazingatia mashauri yote 19, na sio lile moja tu linalosomwa la jimbo la Welezo ambako ACT ilimsimamisha Khamis Mohamed Busara kugombea ubunge. Huyu ni Naibu Katibu Mkuu wa Ngome ya Vijana Taifa.

Majimbo mengine ni ambayo matokeo yake yanapingwa mahkamani: Tumbatu, Nungwi, Kijini, Mkwajuni, Chaani, Bumbwini, Mtoni, Mwera, Paje, Pangawe, Mwanakwerekwe, Kiembesamaki, Dimani, Mpendae, Malindi, Chumbuni, Shaurimoyo na Amani.

ACT pia inapinga matokeo ya ubunge ya majimbo 14 yalioko Pemba ambayo ni Wete, Gando, Kojani, Micheweni, Konde, Wingwi, Ole, Ziwani, Wawi, Chake Chake, Chonga, Kiwani, Chambani na Mkoani.

Kwa upande wa Pemba, mashauri yote 14 yanasubiri uamuzi wa Jaji Mkuu wa Zanzibar kufuatia hatua ya Naibu Mrajis wa Mahkama Kuu Pemba, Chausiku Kuya, kuamua kuyapeleka majalada yote kwake, licha ya kuwepo hoja isiyoamuliwa ya upande wa walalamikaji. Ilihusu uhalali wa kuwepo mawakili kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa SMZ.

About The Author

error: Content is protected !!