Rais Samia Suluhu Hassan
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kwa mkuu wa mkoa wa Morogoro, Adam Malima, kufuatia vifo vya watu 10 vilivyotokana na ajali ya barabarani iliyotokea tarehe 31 Desemba 2025 mkoani humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo tarehe 2 Januari 2026 na mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais, Ikulu, na kueleza kuwa ajali hiyo ilitokea katika Kijiji cha Maseyu, Kata ya Gwata, Wilaya ya Morogoro, kwenye barabara kuu ya Morogoro ikihusisha basi la abiria na lori la mizigo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa basi la abiria lenye namba za usajili T 1662 DMD, aina ya Mitsubishi Fuso, mali ya Kampuni ya Bil Mawio, lilikuwa likisafiri kutoka Morogoro kuelekea Tanga, liligongana uso kwa uso na lori la mizigo aina ya HOWO lenye namba T 956 ELW, mali ya Kampuni ya Kikori, na kusababisha madhara makubwa.
Kufuatia ajari hiyo jeshi la polisi limebainisha waliofariki dunia ni wanawake wawili na wanaume wanane, wote wakiwa ni abiria wa basi hilo. Aidha, jumla ya watu 23 walijeruhiwa katika ajali hiyo na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu, ambapo majeruhi 11 walilazwa na wengine 12 waliendelea kupatiwa matibabu.
Imeelezwa kuwa miili tisa ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro, huku mwili mmoja ukiwa umehifadhiwa katika Kituo cha Afya Mikese. Kati ya miili hiyo, mitano imetambuliwa na kukabidhiwa kwa ndugu, huku mingine ikiwa bado haijatambuliwa kutokana na hali ya majeraha. Wataalamu wa uchunguzi wa vinasaba (DNA) wamechukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Rais Samia ametoa pole kwa familia za marehemu na kuziombea roho za wapendwa wao zipumzike kwa amani, sambamba na kuwatakia uponyaji wa haraka majeruhi wote, pamoja na kuwataka madereva na watumiaji wote wa barabara kuzingatia kikamilifu sheria na kanuni za usalama barabarani.
ZINAZOFANANA
Samia: Tutafanya maridhiano 2026
Gwajima aibuka upya
Mvua zavuruga usafiri wa SGR