MWAKILISHI wa Jimbo la Mtambwe, Dk. Mohamed Ali Sleiman, ameendelea kuonesha ubora na uongozi wenye maono kwa vitendo, kupitia kusaidia upatikanaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba 15 za makazi kwa mayatima na wajane katika awamu ya kwanza ndani ya Jimbo la Mtambwe. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Mradi huu ni sehemu ya juhudi za makusudi za kuinua ustawi wa jamii kwa kuwagusa moja kwa moja walio katika mazingira magumu.
Kupitia mradi huu, tayari familia 8 zimeshahamia rasmi katika kijiji kipya cha makazi hayo, zikiwa na jumla ya watoto 30 wanaoishi katika mazingira salama, yenye heshima na utulivu.
Kwa mujibu wa mpango wa kituo hicho, kitakapokamilika kikamilifu kitaweza kuhudumia watoto wasiopungua 60, wakilelewa katika familia 15 kwa mfumo wa kifamilia unaojenga malezi bora, upendo na mshikamano wa kijamii.
Ujenzi wa nyumba hizo umeleta faraja kubwa kwa wajane na walezi wa mayatima, ambao awali walikosa sehemu sahihi na salama za makazi.
Licha ya ukweli kuwa ujenzi umefadhiliwa, nyumba hizo zimekabidhiwa rasmi kuwa milki ya wajane hao, kwa lengo la kuwawezesha kulea watoto yatima kwa uhakika na hadhi stahiki.
Hatua hiyo imepokelewa kwa shukrani kubwa na wananchi, wakieleza kuwa ni mfano wa uongozi unaoweka utu na haki mbele.
Mbali na makazi, wakaazi wa kijiji hicho watanufaika kwa kupatiwa ujuzi wa maisha na ujasiriamali, ikiwemo kilimo cha mboga mboga na ufugaji, kwa lengo la kuwawezesha kujikimu na kujitegemea kiuchumi.
Mpango huu unalenga kujenga msingi wa maendeleo endelevu badala ya utegemezi.
Aidha, eneo hilo tayari lina msikiti unaowawezesha watoto kufanya ibada na kujifunza Qur’ani, hatua inayokamilisha malezi ya kimwili, kiakili na kiroho.
Wananchi wa Jimbo la Mtambwe wameeleza kuridhishwa kwao na hatua hizi, wakisema kuwa maendeleo ya aina hii ndiyo yanayopaswa kuigwa na viongozi wengine.
Hakika, mradi huu unaendelea kuthibitisha kuwa uongozi wa Dk. Mohamed Ali Sleiman umejikita katika vitendo, huruma na maono ya muda mrefu, kwa lengo la kujenga jamii imara yenye usawa, matumaini na mustakabali bora kwa vizazi vijavyo.
ZINAZOFANANA
Maaskofu Kanisa Katoliki wazidi kucharuka
TMA yatahadharisha kuwapo mvua kubwa
Watumishi TEMESA wafutwe kazi – Mwigulu