Luhaga Mpina, Mgombea Urais wa ACT Wazalendo
LUHAGA Joelson Mpina, amekanusha taarifa kuwa uhusiano wake na chama chake cha ACT-Wazalendo, umekuwa mashakani. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).
“Hakuna kitu kama hicho. Uhusiano wangu na ACT-Wazalendo na viongozi wake, ni mzuri sana,” ameeleza Mpina na kuongeza, “watu wasiumbe maneno kwa jambo lisilokuwapo.”
Mpina alitoa kauli hiyo, wakati akijibu swali la mwandishi wa MwanaHALISI Online, aliyetaka kufahamu juu ya uhusiano wake na chama chake.
Swali la mwandishi lilitokana na hatua ya baadhi ya maofisa wa ACT-Wazalendo, makao makuu, kumzuia mwanasiasa huyo, kutumia kumbi za mikutano za chama hicho, kuzungumza na waandishi wa habari.
Mpina aliyejiunga na ACT-Wazalendo, kutokea Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuteuliwa kuwa mgombea urais wa chama hicho, katika uchaguzi mkuu uliyopita, alipanga kukutana na waandishi wa habari, makao makuu ya chama hicho, wiki iliyopita.
Hata hivyo, muda mfupi kabla ya mkutano huo kufanyika, afisa mmoja wa makao makuu wa chama hicho, alituma ujumbe kwa waandishi uliowajulisha kutofanyika kwa mkutano huo.
Mkutano kati ya waandishi na Mpina, ulipangwa kufanyika katika ukumbi wa Juma Duni Haji, uliyopo makao makuu ya chama hicho.
Ujumbe wa afisa huyo kwa waandishi ulisema yafuatayo: “Dharura. Kwa sababu zilizo nje ya uwezo wetu press (mkutano na waandishi wa habari), uliyokuwa ufanyike muda huu wa saa sita, leo tarehe 05 Desemba 2025, umehairishwa. Samahani kwa usumbufu uliojitokeza.”
Muda mfupi baadaye, waandishi wa habari walijulishwa na msaidizi wa habari wa Mpina, aliyefahamika kwa jina la Benidict Kaguo, ambaye alikuwapo makao makuu ya ACT-Wazalendo, wakati ujumbe wa kughairisha mkutano unatolewa, alieleza kuwa mkutano huo sasa utafanyika Peacock hoteli, saa tisa alasiri.
Mpina alijiunga na ACT- Wazalendo, tarehe 5 Agosti na kupitishwa kuwa mgombea urais, tarehe 6 Agosti 2025, kupitia mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, hakushiriki katika uchaguzi huo, baada ya kuenguliwa na tume ya uchaguzi kwa madai ya kuwekewa pingamizi na Msajili wa Vyama vya Siasa.
ZINAZOFANANA
Jiji kubwa, changamoto kubwa: Uhaba wa maji waitesa Dar
Rais Samia aongoza waombolezaji ibada ya mazishi ya Jenesta
GEN Z ni kina nani, mbona mnatutesa hivi?