December 10, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Kesi kupinga uchaguzi Zbar zaanza

 

WANACHAMA 17 wa ACT Wazalendo waliogombea uwakilishi kwenye Uchaguzi Mkuu Zanzibar wamewasilisha maombi rasmi ya kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyowatangaza washindani wao kutoka Chama Cha Mapinduzi [CCM] kuwa ndio washindi. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Mbele ya Mahakama Kuu ya Zanzibar leo Jumatano, Naibu Mrajis wa Mahkama hiyo, Faraji Shomari Juma alisema tayari walalamikiwa wamejibu madai ya waombaji na kinachofuata ni kusubiri kesi hizo kupangiwa majaji wa kuzisikiliza.

Naibu Mrajis Faraji wakati akielekea kutaka kuakhirisha kesi, upande wa waombaji kulitoka hoja ya kupatiwa hati za majibu ya walalamikiwa ili kufanya masawazisho kama ikihitajika.

“Mhe tunaomba Mahkama iruhusu sasa tupate wasaa wa kupitia majibu ya wenzetu walalamikiwa na kuona kama tunalazima ya kufafanua chochote,” alieleza Wakili Rajab Abdalla Rajab akiwa mmoja ws wanajopo wanaowakilisha waombaji.

Naibu Mrajis Faraji aliridhia hoja hiyo pamoja na indhari ya upande wa walalamikiwa wakihofia kuwa nafasi wanayopewa waombaji kupitia majibu isije ikaathiri mwenendo wa kesi.

“Tutoe indhari kwamba yasije yakatumika majibu yetu kwao waombaji kurekebisha madai yao,” Mbarouk Suleiman Othman akiwakilisha walalamikiwa.

Hoja hiyo ya indhari ilijibiwa na waombaji kwa kueleza mahkama kuwa hawana cha kujibu nje ya yale majibu waliyopokea kutoka kwa walalamikaji hususan kwa sababu “upande wetu hatuna cha kubadilisha au kuongeza.”

Kwa mujibu wa Naibu Mrajis Faraji, Mahkama haina tatizo na indhari hiyo na kwamba inaelekeza waombaji watumie siku saba zijazo kutekeleza walichotaka.

Aliakhirisha kesi akisema watarudi tarehe 18 Disemba 2025 kwa ajili ya kuendelea na hatua muhimu nyengine ya kuyawasilisha majalada kwa Jaji Mkuu Khamis Ramadhan Abdalla Shaaban kwa ajili ya kupanga majaji wa kusikiliza mashauri yote.

Kesi zilizoanza leo ni za majimbo 15 ambayo ni Amani, Mwanakwerekwe, Pangawe, Malindi, Mpendae, Chumbuni, Mtoni, Welezo, Mwera, Chaani, Mkwajuni, Bumbwini, Kijini, Nungwi na Tumbatu.

Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu wa ACT Wazalendo, Omar Said Shaaban anayeratibu malalamiko ya wanachama, kesi zinazohusu majimbo ya Makunduchi, Wilaya ya Kusini Unguja na Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi B, Unguja zitatajwa tarehe 15 Disemba.

Hatua hii inafuatia msimamo wa ACT Wazalendo kinachopinga ukiukwaji mkubwa taratibu za uchaguzi huru na wa haki. Uchaguzi mkuu ulifanyika nchini kote tarehe 29 Oktoba 2025.

Chama hicho pia kimefungua kesi kupinga matokeo ya uwakilishi katika majimbo manane ya kisiwani Pemba – Kojani, Micheweni, Wawi, Chake Chake, Chonga, Kiwani, Chambani na Mkoani.

Pia kwa ubunge kimefungua mashauri kuhoji matokeo ya majimbo 19 Unguja na 14 Pemba.

About The Author

error: Content is protected !!