December 6, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mwanasheria wa kimataifa ataka Tanzania isifukuzwe Jumuiya ya Madola

Rais Samia Suluhu Hassan

 

MWANASHERIA wa kimataifa wa haki za binadamu, Robert Amsterdam, ametoa wito wa dharura kwa Jumuiya ya Madola (Commonwealth), kuisimamisha Tanzania mara moja uanachama wake, kutokana na ukiukaji mkubwa wa maadili ya kidemokrasia kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba 2025. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).

Akiandika kupitia mtandao wa X, Amsterdam ameinukuu kauli rasmi ya mawaziri (CMAG) wa jumuiya hiyo, ambaoo wameiweka Tanzania kwenye kipindi cha majaribio (probation) kutokana na mauaji ya waandamanaji; kuzima mtandao wa intaneti na vikwazo vya uhuru wa kukusanyika na kujieleza.

Kikundi cha mawaziri hao, wametaka Serikali ya Tanzania kufanya marekebisho makubwa kabla ya Machi 2026, vinginevyo watashinikiza kufukuzwa kabisa katika Jumuiya hiyo.

Maandamano ya siku 3 kuanzia tarehe 29 Oktoba 2025, siku ya uchaguzi, yameacha alama kubwa inayoashiria mpasuko wa kisiasa nchini humo.

Katika maandamano hayo, watu kadhaa wamepoteza maisha, huku uharibifu mkubwa wa mali za umma na binafsi ukifanywa, ikiwemo ofisi za chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wiki mbili zilizopita, Jumuiya ya Madola ilitangaza kuanza mchakato wa kusaidia juhudi za maridhiano nchini Tanzania, na ikamtuma Rais wa zamani wa Malawi, Dk. Lazarus Chakwera, kufanya kazi hiyo.

Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya jumuiya hiyo zinasema, mjumbe huyo maalum wa katibu mkuu, aliyetarajiwa kuwasili nchini

tarehe 18 Novemba, hakuweza kuingia nchini Tanzania, kutokana na kile kinachoitwa, “Serikali kuunda tume yake ya uchunguzi.”

Wito wa Amsterdam unakuja wakati vijana kupitia mitandao ya kijamii, wakipanga maandamano mengine makubwa Jumanne ijayo.

Iwapo uamuzi wa kuliondoa taifa hili la Afrika Mashariki kwenye jumuiya hiyo utafikiwa, hilo litakuwa pigo kubwa kwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwani Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekuwa mwanachama mwaminifu wa jumuiya hiyo, tangu mwaka 1961 baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Jumuiya ya Madola – Commonwealth of Nations – ni muungano wa nchi mbalimbali zilizokuwa hasa koloni la Uingereza.

Takribani asilimia 30 ya watu wote duniani, huishi katika nchi wanachama za Jumuiya ya Madola; manufaa makubwa ya kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo, ni nafuu ya kiuchumi.

About The Author

error: Content is protected !!