Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi
RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, amemtaka mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, kuacha mara moja, vitisho dhidi ya Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini (TEC), Padri Charles Kitima. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Katika taarifa yake kwa umma, aliyoitoa jana Ijumaa, tarehe 5 Desemba, Mwabukusi amesema, kauli za Chalamila, zinazochochea ukiukwaji wa haki za binadamu nchini.
Amesema, “Chalamila anatakiwa kukumbushwa kuwa yeye ni miongoni mwa viongozi waliohusika kuchochea matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya raia wakati wa uchaguzi uliyopita, na hivyo hatavumiliwa tena kuendeleza vitisho dhidi ya watu wasio na hatia.
“Shambulio dhidi ya mmoja wetu ni shambulio dhidi ya sisi sote,” ameeleza rais huyo na kuongeza, “…hatutakubali tena, kile kilichomtokea Lissu (Tundu Lissu), mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mmoja wa mawakili mashuhuri nchini, kitokee kwa viongozi wa dini au raia yeyote.
Lissu alishambuliwa kwa risasi, nyumbani kwake, Area D, mjini Dodoma na wanaoitwa na serikali, “watu wasiofahamika.” Alikuwa akirejea nyumbani, kutokea bungeni, alikokuwa amehudhuria mkutano wa Bunge wa asubuhi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mita janja za umeme kwa wateja wa Tanesco mkoani Dar es Salaam, Chalamila alimuagiza mkurugenzi mkuu wa shirika la la umeme la taifa (Tanesco), Lazaro Twange, kumfungulia mashitaka Padre Kitima, kutokana na madai yake kuwa shirika hilo la umma, lilizima umeme, muda mfupi kabla ya yeye kushambuliwa.
Chalamila alisema, alimsikia Padre Kitima, akieleza kwamba siku aliyovamiwa kulikuwa na mpango kati ya wavamizi na Tanesco, na kwamba shirika hilo, lilizima umeme ili wahalifu waweze kumdhuru kwa haraka.
Kwa mujibu wa Mwabukusi, kuna ushahidi wa kutosha wa kauli na matendo ya Chalamila kabla na baada ya uchaguzi, zinazoweza kuchukuliwa kama uchochezi wa mauaji ya kimbari, na sasa ni wakati wa kuchora mstari.
Amesema, TLS imepanga kumchukulia hatua rasmi Chalamila na wote wanaoshirikiana naye kuendeleza matendo ya kinyanyasaji dhidi ya raia kwa kisingizio cha sheria.
Padre Charles Kitima, alishambuliwa akiwa ndani ya makao makuu ya TEC, Kurasini jijini Dar es Salaam, tarehe 1 Mei mwaka huu.
Mara baada ya shambulio hilo, Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, lilitangaza kumshikilia Rauli Mahabi, mkazi wa Kurasini, likimtuhumu kuhusika na shambulio hilo.
Hata hivyo, mpaka sasa, Mahabi hajafikishwa mahakamani na wala jeshi hilo, halijaelezwa uchunguzi wa suala hilo, umefikia hatua gani.
ZINAZOFANANA
Chalamila: Tanesco mchukulieni hatua Dk. Kitima
Uwezekano wa wanawake kuwa Mashemasi bado mgumu
Mabalozi wa magharibi wataka uchunguzi huru wa mauaji ya 29 Oktoba