November 20, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Serikali yaanza kuonja kibano cha kimataifa

Bunge la EU

 

BUNGE la Jumuiya ya Ulaya (EU), limepitisha kwa wingi, pingamizi dhidi ya mpango wa Tume ya Ulaya wa kuelekeza msaada wa kifedha kwa Serikali ya Tanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hatua hiyo imekuja baada ya matokeo ya kura zilizopigwa na Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Ulaya juu ya kuzuia utekelezaji wa mpango wa kuipatia Tanzania mamilioni ya fedha kutoka umoja huo.

Kwa uamuzi huo, mamilioni ya fedha kutoka mfuko wa NDICI-Global Europe – sasa hazitaletwa nchini.

Kuzuiliwa kwa fedha hizo, kunatokana na tuhuma za kushamiri kwa vitendo vya haki za binadamu nchini Tanzania, pamoja na kuminya demokrasia.

Haya yanajiri wiki tatu baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, tarehe 29 Oktoba; uchaguzi uliokuwa umegubikwa na maandamano na ghasia.

Katika upigaji kura uliofanyika, wajumbe 53 walikubali kuiwekea Tanzania pingamizi huku wawiki wakikataa na mmoja kutokuwa na upande.

Tume ya Ulaya ilipanga kutuma zaidi ya Euro 150 milioni katika mwaka ujao wa 2026, kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maendeleo, fedha zinazoweza kuelekezwa kwingine.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Bunge la Ulaya limesema, utekelezaji wa msaada huo haukuzingatia hali halisi ya haki za binadamu na utawala wa sheria nchini Tanzania.

Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge hilo, David McAllister amesema, uamuzi huo ni ishara ya wazi kwamba Umoja wa Ulaya hauwezi kuendelea kutoa fedha kwa misingi ya nyaraka zinazopuuza hali ya ukandamizaji wa kisiasa, uchaguzi usio wa haki, na mwenendo wa kiimla wa Serikali.

“Hii inaweza kuathiri vibaya mipango ya misaada ya EU nchini Tanzania mwaka 2026 na kuonyesha mgawanyiko mkubwa kati ya Bunge la Ulaya na Tume ya Ulaya katika masuala ya sera za kigeni na maendeleo,” ameeleza mwanadiplomasia mmoja jijini Dar es Salaam.

Juzi Jumanne (tarehe 18 Novemba 2025), Rais Samia Suluhu Hassan, alinukuliwa akisema, matukio yaliyojitokeza hivi karibuni yameathiri taswira ya nchi kimataifa, hasa katika masuala ya kifedha na uwezo wa serikali kupata mikopo kutoka kwa taasisi za kimataifa.

Alikuwa akirejea ghasia za maandamano ya siku tatu za uchaguzi wa 29 Oktoba 2025, yaliyosababisha vifo vya watu kadhaa na uharibifu wa mali za umma na binafsi.

Alitoa kauli hiyo wakati wa kuapisha baraza lake jipya la mawaziri katika Ikulu ya Chamwino.

Alisema, uchumi wa Tanzania bado unategemea kwa kiwango kikubwa mikopo ya nje, na kwamba sintofahamu ya kisiasa iliyojitokeza inaweza kupunguza imani ya taasisi hizo.

Akaongeza, “Rasilimali zetu ni chache, mara nyingi tunategema kupata kutoka nje, mikopo kutoka kwa taasisi mbalimbali, za kimataifa, mabenki ya kimataifa, lakini yaliyotokea nchini kwetu, yametutia doa kidogo, kwa hiyo huend ayakatupunguzia sifa ya kupata hiyo mikopo kwa urahisi kama tulivyopata muhula wa kwanza” wa urais wake.

About The Author

error: Content is protected !!