November 20, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mtanzania aliyeuawa Israel azikwa

 

MAZIKO ya Joshua Loitu Mollel, raia wa Tanzania, aliyefariki dunia, tarehe 7 Oktoba 2023, nchini Israel, baada ya kushambuliwa na kundi la wanamgambo wa Hamas, yamefanyika leo, 20 Novemba 2025, nyumbani kwao, wilayani Simanjiro mkoani Arusha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mabaki ya mwili wa Joshua yalirejeshwa nchini jana, kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), miaka miwili baada ya mauaji hayo. Ulipokelewa na familia pamoja na maafisa wa serikali.

Alishambuliwa na kuuawa huko Nahal Oz, eneo la kusini mwa Israel. Joshua alifika Israel wiki tatu kabla ya kuuawa na Hamas.

Mwili wake ulitekwa na washambuliaji na kupelekwa Ukanda wa Gaza.

Maziko hayo yalihudhuriwa na viongozi wa serikali, viongozi wa dini, wananchi wa maeneo mbalimbali pamoja na mwakilishi wa ubalozi wa Israel nchini.

Familia yake, ndugu na jamaa walijitokeza kwa wingi kumuaga kijana huyo aliyekwenda nchini Israel kwa ajili ya mafunzo ya kilimo.

Kabla ya kusafirishwa kutoka Israel, ubalozi wa Tanzania nchini humo uliandaa ibada maalum ya kumuaga katika mnara wa kumbukumbu wa Tel Aviv.

Serikali ya Israel ilithibitisha kurejeshwa kwa mabaki ya mwili wake, mnamo 19 Novemba 2025, chini ya makubaliano ya usitishaji mapigano yaliyosimamiwa na Marekani.

Baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu katika kituo cha kitaifa cha uchunguzi wa vinasaba, familia iliithibitishiwa rasmi kuwa mabaki hayo ni ya Joshua.

Katika makubaliano hayo, Hamas ilirejesha miili ya mateka 19 wa Israel pamoja na miili ya raia watatu wa kigeni – Thailand, Nepal na Joshua kutoka Tanzania, huku Israel ikikabidhi miili ya Wapalestina 285.

Hadi sasa, miili ya mateka sita, Waisraeli watano na raia mmoja wa Thailand inaendelea kushikiliwa huko Gaza.

“Mazishi ya Joshua yamehitimisha safari ndefu na yenye uchungu kwa familia yake, ambayo kwa miaka miwili imekuwa ikisubiri uthibitisho na hatimaye kurejeshwa kwa mabaki ya mpendwa wao,” ameeleza Christopher ole Sendeka, mbunge wa zamani wa Simanjiro.

Katika mapambano hayo, mamia ya wananchi wameuliwa.

About The Author

error: Content is protected !!