November 14, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Samia atangaza msamaha kwa waandamanaji

 

RAIS Samia Suluhu Hassan, ametangaza msamaha kwa vijana waliokamatwa, kufuatia maandamano ya siku tatu kuanzia siku ya uchaguzi mkuu wa 29, Oktoba. Anaripoti Saed Kubenea, Dar es Salaam … (endelea).

Alisema, “Ninatambua kwamba vijana wengi waliokamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhaini, hawakujua wanachokifanya.”

Aliongeza, “Nikiwa mama na mlezi wa taifa hili ninavielekeza vyombo vya sheria na hasa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuangalia kiwango cha makosa kilichofanywa na vijana wetu kwa wale ambao wanaonekana walifuata mkumbo na hawakudhamiria kufanya uhalifu, wawafutie mashitaka.”

Katika kutekeleza hilo, Rais amemuagiza Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai nchini Tanzania (DPP), kuwafutia mashitaka ya uhaini, vijana wote ambao wataona walifuata mkumbo kwenye maandamano hayo.

Rais Samia alitoa kauli hiyo, wakati akifungua Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mjini Dodoma, Ijumaa ya tarehe 14 Novemba mwaka huu.

Kwa mujibu wa Ibara ya 91(1) ya Katiba, Rais Samia alisema kuwa vijana hao wengine walifuata mkumbwa hivyo waachiwe kwa utaratibu na kurejeshwa kwa familia zao.

Akawaomba kuacha kushawishiwa kuchoma nchi yao kwa mikono yao wenyewe, akidai kuwa vijana ndio walinzi na walezi wa taifa.

Amesema, serikali yake, imeunda tume maalum itakayochunguza yale yaliyotokea tarehe 29 Oktoba, ili kujua kiini cha tatizo ambapo taarifa hiyo itatuongoza kujielekeza kwenye mazungumzo ya kuleta maelewano.

Rais Samia pia alitangaza kuwa serikali imeunda tume maalumu kuchunguza matukio yaliyotokea wakati wa maandamano hayo.

Akizungumzia kipaumbele cha serikali atakayounda, Rais amesema, itafanyia mabadiliko Katiba ya Jamhuri ya Muungano iliyopo sasa.

Alisema, waliahidi kuanza kulifanyia kazi mabadiliko ya katiba kwa siku 100 za muhula wa pili, lakini kwa haya yaliyotokea, wataanza na kuunda tume ya usuluhishi na maelewano.

Katika maandamano hayo yaliyodumu kwa siku tatu, kuanzia 29 Oktoba 2025 – siku ya uchaguzi – watu kadhaa wamepoteza Maisha.

Walioandamana walikuwa wakishinikiza kuwapo mabadiliko kwenye mifumo ya uchaguzi na usimamizi wa haki.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Mohammed Thabit Kombo, alinukuliwa akisema, hafahamu idadi halisi ya waliofariki.

About The Author

error: Content is protected !!